Haiti yatangaza hali ya hatari
WANDERI KAMAU na MASHIRIKA
HAITI mnamo Jumatatu, Machi 4, 2024, ilitangaza hali ya hatari kwa muda wa saa 72 na kafyu nyakati za usiku katika jiji kuu la Port-au-Prince, baada ya visa viwili vya wafungwa kutoroka gerezani kutokana na kudorora kwa hali ya usalama.
Wikendi, magenge yaliyojihami vikali yalivamia gereza moja kubwa katika jiji hilo, hali iliyosababisha vifo vya watu 12 huku wengine karibu 4,000 wakiachiliwa huru.
Viongozi wa magenge hayo walisema wanataka kumlazimisha Waziri Mkuu Ariel Henry kujiuzulu.
Kwa sasa, kiongozi huyo yuko nje ya taifa hilo.
Kulingana na taarifa ya serikali, magereza mawili—moja lililo katika jiji la Port-au-Prince na jingine katika mji wa Croix des Bouquets—yalivamiwa wikendi.
Miongoni mwa wale walikuwa wakizuiliwa katika magereza hayo ni viongozi wa magenge walioshtakiwa kuhusiana na mauaji ya aliyekuwa rais wa taifa hilo, Jovenel Moïse, mnamo 2021.
Ongezeko la ghasia nchini humo lilianza Alhamisi wiki iliyopita, baada ya Bw Henry kusafiri humu nchini kujadili mpango wa Kenya kusafirisha kikosi cha polisi 1,000 katika taifa hilo na Rais William Ruto.
Polisi hao watakuwa sehemu ya kikosi cha kimataifa kitakachotumwa na mataifa kadhaa kuisaidia serikali ya taifa hilo kuyakabili magenge ya uhalifu.
Tangazo la kumwondoa Bw Henry mamlakani lilitolewa na kiongozi wa genge Jimmy Cherizier (maarufu kama “Barbeque”).
“Sisi sote, makundi yaliyojihami katika miji ya mikoa na makundi yaliyojihami katika mji mkuu, tumeungana,” akasema Chérizier, ambaye ni polisi wa zamani.
Idara ya Polisi nchini humo ilikuwa imeliambia jeshi kulisaidia kudhibiti hali ya usalama katika gereza kuu jijini Port-au-Prince, ijapokuwa makundi yaliyojihami yalilivamia mnamo Jumamosi.
Mnamo Jumapili, milango ya gereza hilo bado ilikuwa wazi, na hakukuwa na dalili zozote za uwepo wa maafisa wa ulinzi. Ripoti zilieleza kuwa wafungwa watatu waliojaribu kutoroka waliuawa.
Mfanyakazi mmoja katika gereza hilo aliwaambia wanahabari kwamba wafungwa 99 waliamua kubaki gerezani kwa kuhofia kuuawa.