Hakikisho la usalama kutoka kwa Trump laipa moyo Ukraine
UKRAINE na wandani wake barani Ulaya wametiwa matumaini na ahadi ya Rais Donald Trump (pichani) ya kutoa hakikisho la usalama kwa nchi hiyo kumaliza vita kati yake na Urusi.
Licha ya kushaajishwa na rais huyo wa Amerika, Ukraine na nchi za Ulaya bado hazijui iwapo Urusi itaridhia msimamo wa Trump.
Mnamo Jumatatu, Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky alikutana na Trump katika Ikulu ya White House na alisema mkutano huo ulifana kabisa, akieleza imani yake kuwa uhasama kati ya Ukraine na Urusi utaisha.
Akiwa ameandamana na viongozi kutoka Ujerumani, Ufaransa na Uingereza, Zelensky alipokelewa kwa mbwembwe na Trump kinyume na mapokezi ya Februari ambapo viongozi hao wawili walijibizana vikali.
Urusi bado haujazungumzia mkutano wa Trump na Zelensky japo nia ya Trump ni kuwa mkutano utakaofuata pia utamshirikisha Rais Vladimir Putin.
Waziri wa Masuala ya Nje wa Urusi Sergei Lavrov alisema kuwa mkutano wowote ambao utashirikisha viongozi wote watatu lazima uibuke na mapendekezo ambayo yatahakikisha matakwa ya Urusi yanatimizwa.