• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 11:33 PM
Hatua ya UN ‘kuhalalisha’ bangi yasifiwa na wengi

Hatua ya UN ‘kuhalalisha’ bangi yasifiwa na wengi

Na MASHIRIKA

GENEVA, Uswisi

WANAHARAKATI ambao kwa miaka mingi wamekuwa wakitetea matumizi ya bangi, Alhamisi walisifu hatua ya Umoja wa Mataifa kuondoa mmea huo katika orodha ya dawa hatari za kulevya.

Tume ya Umoja wa Mataifa inayosimamia masuala ya mihadarati iliidhinisha pendekezo la Shirika la Afya Duniani (WHO) la kuondoa bangi katika kundi la dawa za kulevya linalojumuisha mihadarati mingine kama vile heroin.

Hata hivyo, dawa hiyo ingali katika orodha ya dawa za kulevya ijapokuwa imeshushwa daraja, na mataifa yangali huru kujiamulia kuhusu jinsi ya kudhibiti matumizi yake.

Mchanganuzi tajika kuhusu masuala ya matumizi ya dawa za kulevya, Alfred Pascual alisifia hatua hiyo ambayo sasa itarahisisha uwezo wa mataifa kuidhinisha bangi itumiwe kama tiba, akisema dawa hiyo si hatari jinsi ambavyo imekuwa inadaiwa.

“Tumefumbwa macho na madai kwamba bangi ni hatari hasa kwa muda wa miaka 60 iliyopita. Hatua ya UN kuidhinisha pendekezo la WHO ni nzuri sana na ya kusifiwa,” akasema.

Uamuzi huo ulichukuliwa kwa kuwa tafiti nyingi zimebaininisha kuwa bangi ni tiba kwa baadhi maradhi yanayosumbua binadamu.

Tangu mnamo 1961, bangi imekuwa kati ya dawa za kulevya zinazooredheshwa kuwa hatari zaidi ambazo zinaleta uraibu mwilini zikitumiwa kila mara na binadamu.

Orodha hiyo huwa imejumuisha dawa nyingine hatari kama heroini na kokeni ambazo matumizi yake yamepigwa marufuku katika nchi kadhaa duniani.

WHO mnamo Jumatano ilipendekeza hatua hiyo ichukuliwe kwa kuwa imebainika kuwa bangi si hatari sana kwa maisha ya binadamu badala yake ni tiba kwa maradhi sugu.

Hatua hiyo ya UN imeshabikiwa na mashirika mbalimbali ambayo yalisisitizia umuhimu wa bangi kama dawa ya kulevya.

“Hatua hii ilifaa ichukuliwe mapema kwa kuwa bangi ni dawa. Ingawa bangi imeondolewa kwenye kitengo cha dawa za kulevya, UN inafaa kuhakikisha kuwa hata mataifa mbalimbali yanaiondoa kwenye kundi la dawa za kulevya,” akasema Anne Fordham ambaye ni Mkurugenzi Mkuu wa Sera za Kimataifa kuhusu kupambana na dawa za kulevya.

Ingawa bangi imeondolewa kama dawa ya kulevya, huenda itachukua muda kwa serikali mbalimbali kuruhusu raia wake waitumie tu kwa sababu za kimatibabu.

Hata hivyo, nchi kadhaa ambazo hutegemea ushauri wa UN nazo zitaikumbatia japo tu kama tiba wala si kuwaruhusu raia waitumie kwa burudani.

Kwenye kikao cha Jumatano, mataifa 27 yalipiga kura kuunga bangi kuondolewa kama dawa ya kulevya huku 25 yakipinga.

Marekani, Ujerumani na Afrika Kusini ni kati ya nchi zilizounga mkono pendekezo hilo huku Brazil, Urusi, Pakistan na Uchina zikipinga.

Hata hivyo, mataifa wanachama walipinga mapendekezo mengine ya WHO kuhusu matumizi ya bangi ambayo huenda yakawaathiri wanaoitumia kando na kutibu maradhi.

You can share this post!

ODM kifua mbele Msambweni – Utafiti

TAHARIRI: Vyuo vitafute karo zaidi kwingineko