Kimataifa

Hii PSG itabidi tuwe wajanja – Arteta

Na MASHIRIKA May 1st, 2025 Kusoma ni dakika: 2

LONDON, UINGEREZA

ARSENAL itahitaji kufanya kazi ya ziada itakapokutana na PSG katika mechi ya marudiano ya nusu fainali ya Klabu Bingwa barani Ulaya juma lijalo ugani Parc des Princes jijini Paris.

Kwenye mechi hiyo ya marudiano, wenyeji PSG wataingia uwanjani wakiwa kifua mbele kwa ushindi wa bao moja lililofungwa na Ousmane Dembele ugani Emirates, Jumanne usiku.

Sherehe za mashabiki wa The Gunners kufurahia bao la kusawazisha dakika ya 47 zilikatizwa haraka baada ya mtambo wa VAR kukataa bao hilo kwa madai kuwa mfungaji Mikel Merino alikuwa ameotea.

Akizungumza kuhusu mechi hiyo ya Jumanne, kocha Mikel Arteta alisema alisikitika na matokeo hayo kutokana na bao la mapema la Dembele ambaye alikuwa mwiba kwenye lango la wenyeji.

Arteta alisema vijana wake walikuwa na nafasi nyingi za kufunga mabao lakini hawakuzitumia, huku juhudi za Gabriel Martineli na Leandro Trossard zikivurugwa na kipa matata Gianluigi Donnarumma wa timu ya taifa ya Italia.

“Tulilemewa dakika 15 za kwanza lakini tukacheza vizuri katika kipindi cha pili, ingawa hatukufanikiwa kupata bao.”

“Kufuzu kwa fainali ya Klabu Bingwa lazima mtu azidishe juhudi zake na kucheza kwa kiwango cha juu. Itabidi tufanye hivyo tutakaporudiana juma lijalo.”

“PSG ni miongoni mwa timu bora, ikikumbukwa kuwa wameshinda timu zote za Uingereza msimu huu. Si rahisi kuwashinda. Itabidi tutumie mbinu tofauti ili tuwashinde.”

Kilikuwa kichapo cha mara ya 18 kwa Arsenal katika michuano ya bara Ulaya mbele ya mashabiki wao, matokeo ambayo yamepunguza matumaini yao ya kutwaa ubingwa wa Kombe la Klabu Bingwa Ulya kwa mara ya kwanza tangu klabu hiyo ianzishwe mnamo 1886 (miaka 136 iliyopita).

Kipa David Raya wa Arsenal aliungama kwamba bao la PSG lilifungwa kwa ufundi mkubwa, kwani kulikuwa na wachezaji saba wa Arsenal waliojaribu kuzuia.

“Tungeshinda mechi hiyo iwapo tungetumia nafasi tulizopata vizuri. Walipata nafasi yao na wakaitumia vizuri. Ugenini, tutajitahidi. Naamini tunaweza kushinda timu yoyote.”

Luis Enrique wa PSG amebashiriki kuwa fainali itakuwa kati ya vijana wake na Barcelona ambao walipangiwa kucheza na Inter Milan ugani Estadi Olimpic Lluis Companys jana usiku.

Hata hivyo, kocha huyo alionya vijana wake dhidi ya Arsenal ambao walishinda vigogo Real Madrid katika hatua ya robo fainali hapo awali.

Arsenal ilibandua Madrid kwa jumla ya mabao 5-1 na kutinga nusu fainali kwa mara ya kwanza tangu ifanye hivyo mnamo 2009 baada ya kuondoa Manchester United.

Awali, PSG walikuwa wamebandua Liverpool katika hatua ya 16-Bora, Aston Vila kwenye robo fainali, baada ya kutoka nyuma na kushinda Manchester City kwenye hatua ya ligi ya michuano hiyo ya Ulaya.