Kimataifa

Hija yaanza huku washiriki wakielezea hofu ya corona

July 30th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na AFP

MECCA, Saudi Arabia

MAHUJAJI wa Kiislamu jana walianza kushiriki katika hafla ya kila mwaka ya Hija nchini Saudi Arabia, ingawa idadi ya washiriki mwaka 2020 ilikuwa chache kutokana na tishio la janga la virusi vya corona.

Wenyeji wa mji mtakatifu wa Mecca pia walichukua tahadhari kuepuka kuambukizwa na wageni, kwenye hafla itakayodumu kwa siku tano.

Washiriki walikuwa wamevalia barakoa, ikiwa ni mojawapo ya masharti makuu ambayo yametolewa na nchi mbalimbali duniani kudhibiti maambukizi ya virusi.

Hata hivyo, hali ni tofauti mwaka huu kwani ni hadi washiriki 10,000 pekee wanaoishi humo wataruhusiwa kushiriki, kinyume na miaka ya awali, ambapo watu 2.5 milioni hushiriki kila mwaka.

Mahujaji waliingia katika makundi kwenye msikiti wa Grand Mosque, ambao hutumika na washiriki kufanyia maombi.

Kando na kuvalia barakoa, washiriki wanahitajika kuosha mikono na kutokaribiana watakaposhiriki kwenye msururu wa shughuli kadhaa za kidini kwa siku hizo tano.

Kwa kawaida, shughuli hizo hufanyika Mecca na maeneo mengine matakatifu yaliyo viungani mwa mji huo, ambapo washiriki hupata nafasi kuyazuru.

Wale walioteuliwa kushiriki walipimwa viwango vyao vya joto na kuwekwa kwenye karantini kabla ya kuruhusiwa kuanza kuingia mjini humo wikendi iliyopita.Shirika la habari la serikali lilionyesha wahudumu wa afya wakinyunyizia dawa mizigo ya washiriki ili kuua virusi. Baadhi ya washiriki waliwekwa mikanda maalum ya kielektroniki mikononi mwao, ili kuwawezesha maafisa wa serikali kubaini waliko.

Maeneo yaliyo karibu na sehemu takatifu ya Kaaba pia yalinyunyiziwa dawa na wahudumu. Maafisa wanaosimamia hafla waliifunga sehemu hiyo mwaka huu, wakisema washiriki hawataruhusiwa kuigusa ili kupunguza uwezekano wa kueneza virusi. Mikakati mingine muhimu ambayo imewekwa ni uwepo wa kliniki na ambulensi ili kuwashughulikia mahujaji. “Hakuna hofu yoyote ya usalama katika haji ya mwaka huu. Hata hivyo, lengo kuu la kudhibiti idadi ya washiriki ni kupunguza uwezekano wa maambukizi miongoni mwao,” akasema Mkurugenzi wa Usalama wa Umma nchini humo, Khalid bin Qarar Al-Harbi.

Vyombo vya habari vya kigeni pia vimezuiwa kuangazia hafla mwaka 2020. Hili linatokana na kanuni kali ambazo serikali imeweka kwa yeyote anayeingia mjini Mecca.

Awali, maafisa wa serikali walisema ni watu 1,000 wanaoishi nchini humo pekee wangeruhusiwa kushiriki. Licha ya hayo, vyombo vya habari vilisema kuwa karibu watu 10,000 wameruhusiwa.