Kimataifa

Historia mwana wa Rais Biden akipatikana na hatia ya uhalifu

June 12th, 2024 2 min read

NA MASHIRIKA

WASHINGTON DC, AMERIKA

HUNTER Biden, mwana wa Rais wa Amerika amepatikana na hatia ya kumiliki bunduki kinyume cha sheria.

Hii ni kesi ya kwanza ya jinai ya kihistoria kumkabili mtoto wa rais aliye madarakani.

Hunter ambaye ana umri wa miaka 54 alipatikana na hatia kwa makosa yote matatu ya uhalifu yaliyotokana na ununuzi wake wa bunduki mwaka 2018 akiwa mraibu wa dawa ya kulevya.

Uamuzi huo unakuja wakati baba yake akiendelea na kampeni dhidi ya rais wa zamani, Donald Trump.

Rais Biden pia alilazimika kuahirisha ziara yake ya Wilmington, Delaware, mji wa familia yake ambapo kesi hiyo ilikuwa ikisikilizwa.

Baada ya mwanawe kupatikana na hatia, rais huyo alisema kuwa ataendelea kumuunga mkono Hunter liwe liwalo.

Maryellen Noreika ni jaji anatarajiwa kutangaza tarehe ambayo hukumu itatolewa.

Washtakiwa wanaopatikana na hatia katika mahakama ya shirikisho ya Delaware kwa kawaida huhukumiwa ndani ya siku 120 baada ya kupatikana na makosa.

Wiki jana, Hunter Biden alihojiwa kwanza na maafisa wa uangalizi, ambao baadaye walitayarisha ripoti ya siri inayoweka aina mbalimbali za adhabu kulingana na miongozo ya hukumu ya shirikisho.

Hunter Biden Jumanne aliwasili mahakamani kwenye ufunguzi wa kesi ya uhalifu dhidi yake, na ilihusisha ushahidi kutoka kwa wapenzi wake wa zamani na maelezo binafsi kuhusu matatizo yake ya matumizi ya dawa za kulevya.

Mke wa zamani wa Hunter Biden, Kathleen Buhle, pia alitoa ushahidi kuhusu kesi hiyo.

Hallie Biden, mjane wa kaka ya Hunter Biden Beau pia alikuwa kwenye orodha ya mashahidi wa upande wa mashtaka.

Hunter alikuwa akikabiliwa na mashtaka matatu ya uhalifu kutokana na kununua bunduki 2018, wakati ambapo kulingana na rekodi zilizopo, alikuwa mraibu wa dawa za kulevya.

Pia alipatikana na hatia ya kumdanganya muuza bunduki aliyeidhinishwa na serikali kuu, kuwa hakuwa akitumia dawa za kulevya, na akauziwa bunduki.

Kesi hiyo ilifunguliwa baada ya makubaliano ya awali na waendesha mashtaka ya kuahirisha kesi hiyo hadi baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka huu kuvunjika.

Kwa mtoto wa rais kukabiliwa na kesi ya jinai ni jambo lisilokuwa la kawaida kabisa na limempaka tope Biden.

Haya yanajiri siku chache tu baada ya kesi dhidi ya rais wa zamani wa nchi hiyo, Trump ambaye ni mpinzani mkuu wa Biden kuamuliwa.