Kimataifa

Homa hatari China yaibua hofu ya kuzuka janga jingine duniani

July 1st, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na MASHIRIKA

BEIJING, CHINA

AINA mpya ya homa ambayo ina uwezo wa kugeuka kuwa janga la kiafya imegunduliwa na wanasayansi nchini China.

Wanasema homa hiyo ililpuka majuzi na iligunduliwa ndani ya nguruwe, lakini pia inaweza kuathiri wanadamu.

Watafiti wameelezea hofu kuwa, huenda virusi vinavyosababisha homa hiyo vikabadilikana kusambaa kutoka mtu mmoja hadi mwingine, na kuenea kote ulimwenguni.

Ingawa wanasema virusi hivyo sio tishio, vina uwezo wa kuishi ndani ya binadamu na hivyo ipo haja ya kufuatiliwa kwa makini.

Na kwa kuwa virusi hivyo ni vipya, mwili wa binadamu haujajenga kinga dhidi yake.

Wanasayansi waliochangia makala katika jarida la “Proceedings of the National Academy of Sciences” na ambao hufuatilia hali ya virusi hivyo katika nguruwe wanasema, vinafaa kuchunguzwa kwa makini.

Na aina mpya ya virusi vinavyosababisha ugonjwa wa Influenza pia vinafuatiliwa kwa makini na wataalamu wakati huu ambapo ulimwengu unapambana na janga la virusi vya corona.

Mlipuko wa homa ya nguruwe uliotokea mnamo 2009 ndio wa mwisho kuutikisa ulimwengu.

Hata hivyo, homa hiyo haikusababisha maafa makubwa jinsi ilivyohofiwa kwa sababu haikuweza kuwaathiri idadi kubwa ya watu wenye umri mkubwa. Hii ni kwa sababu virusi vya homa hiyo vilifanana na vile ambavyo viliwahi kuenea ulimwenguni katika miaka ya nyuma.

Virusi hivyo kwa jina, A/H1N1pdm09, sasa vimeweza kudhibitiwa kupitia chanjo ambayo hutolewa kila mwaka kuhakikisha watu wanapata kinga.

Homa mpya iliyogunduliwa majuzi nchini China inafanana na homa ya nguruwe ya 2009, japo ina mabadiliko machache mapya.

Kufikia sasa, haijaibua tishio kubwa, lakini Profesa Kin-Chow Chang na wengine ambao wamekuwa wakiifanyia uchunguzi, wanasema ni “homa ambayo inastahili kufuatiliwa kwa makini.”

Virusi vinavyosababisha homa hiyo, ambavyo wanasayansi wanaviita, G4 EA H1N, vina uwezo wa kuzaana katika mishipa ya hewa ndani ya mwili wa binadamu.

Wanasayansi walipata ushahidi mpya wa maambukizi miongoni mwa watu waliokuwa wakifanyakazi katika vichinjio vya nguruwe nchini China. Hii ni baada ya wao kufuatilia data kuanzia 2011 hadi 2018.

Chanjo ya sasa dhidi ya homa mbalimbali haina uwezo wa kuidhibiti.