• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 12:09 PM
Huenda mnichukie lakini lazima tuvamie Rafah, Netanyahu asema

Huenda mnichukie lakini lazima tuvamie Rafah, Netanyahu asema

JERUSALEM, Israel

Na MASHIRIKA

WAZIRI Mkuu wa Israel amesema kuwa tarehe imetengwa ya uvamizi wa mji wa Rafah kusini mwa Gaza huku mazungumzo ya kusitishwa kwa mapigano kati yao na Hamas, yakiendelea Cairo, Misri.

Hata hivyo, dalili za kukamilika kwa mazungumzo hayo, na mwafaka kupatikana, bado hazijajitokeza.

Kwenye taarifa kupitia video ya Kiyahudi, Netanyahu amekariri msimamo wake kwamba shambulio ya ardhini katika Rafah, ambako zaidi ya Wapalestina 1.5 milioni wanaishi, ni muhimu katika azma yao ya kushindi vita hivyo.

Mji wa Rafah unapakana na Misri.

“Itafanyika. Kuna tarehe ambayo imetengwa,” Netanyahu akasema Jumatatu, bila kutoa maelezo zaidi.

Haya yanajiri baada ya Hamas, mwishoni mwa wiki jana, kupewa pendekezo jipya katika mazungumzo hayo ya kusitisha vita.

Lakini pendekezo hilo halionekani kama ambalo litawezesha makubaliano kufikiwa.

Kundi hilo la Kipalestina lilithibitisha, katika taarifa, kwamba linaangalia upya pendekezo hilo, lakini likasema kuwa Israel “haijajibu matakwa yetu kwamba ikome kushambulia watu wetu”.

Msemaji mkuu wa Hamas Sami Abu Zahry aliliambia shirika la habari la Al Jazeera kwamba kauli ya Netanyahu “inaibua maswali kuhusu haja ya kurejelewa mazungumzo”.

“Ufanisi wa mazungumzo yoyote utategemea kukomeshwa kwa mashambulio,” akasema Zahry akiongeza kuwa matakwa ya Hamas ingali kwamba “sharti mashambulio dhidi ya watu wetu yakomeshwe.”

Kufikia sasa, Israel imekataa matakwa ya Palestina kwamba iruhusu kurejea kwa maelfu ya raia wa Gaza katika eneo la kaskazini mwa ukanda huo na iondoe wanajeshi wake kutoka eneo hilo.

Imedumisha vikosi

Hata hivyo, Idara ya Jeshi ya Israel ilisema imeondoa baadhi ya wanajeshi wake wa ardhini kutoka Gaza lakini imedumisha wanajeshi wa kusimamia mkondo wa kutoka mashariki hadi magharibi.

Mkondo huo unagawanya Gaza kuwili na unazuia kurejea kwa Wapalestina eneo la kaskazini.

Amerika inaendelea kupinga, waziwazi, mpango wa Israel kuvamia Rafah. Hii ni kwa sababu, kulingana na Rais Joe Biden, hamna mpango thabiti wa kunusuru idadi kubwa ya raia waliotorokea eneo hilo kutafuta usalama.

Afisa mmoja wa Israel ambaye hakujitambulisha aliambia shirika la habari la AFP kwamba Israel inanunua mahema 40,000 kama sehemu ya maandalizi ya kuwaondoa raia wa Palestina kutoka Rafah.

Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Amerika Mathew Miller aliwaambia wanahabari kufuatia tangazo la Netanyahu kwamba Amerika haijafahamishwa kikamilifu kuhusu mipango hiyo mipya kuhusu Rafah.

“Tumeweka wazi kwa Israel kwamba tunaamini uvamizi wa Rafah utasababisha madhara makubwa kwa raia hao na kwamba mwishowe utaathiri hali ya usalama wa Israeli,” Miller akasema.

Haya yanajiri huku viongozi wa Misri, Jordan na Ufaransa walioandaa taarifa ya pamoja inayohimiza usitishwaji wa mapigano mara moja na bila masharti yoyote.

Taarifa hiyo ilichapishwa katika magazeti mbalimbali makuu kama vile “The Washington Post” na “Le Monde”.

Wito sawa na huo pia ulitolewa katika mkutano wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa (UNSC) mwishoni mwa mwezi jana wa Machi.

  • Tags

You can share this post!

Leteni hao majeruhi Bayern tuwape dozi, Arsenal sasa...

Mudavadi ameza ndoano ya UDA

T L