Kimataifa

ICC sasa yakazia sikio kesi ya kiongozi wa waasi Uganda Joseph Kony

Na REUTERS September 10th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

HAGUE, UHOLANZI

MAHAKAMA ya Kimataifa ya Jinai yenye makao yake Uholanzi (ICC) jana ilianza mkondo wa mwisho wa kukamilisha kusikizwa kwa kesi dhidi ya mwasi mkuu wa kivita nchini Uganda Joseph Kony.

Wachanganuzi wa masuala ya kisheria wanasema kukamilishwa kwa kesi hiyo na uamuzi kutolewa utatoa mwelekeo kwa viongozi wanaoandamwa na ICC kama Waziri Mkuu wa Israeli Benjami Netanyahu na Rais wa Urusi Vladimiri Putin.

Iwapo Kony atafungwa au kupewa adhabu kali, Netanyahu na Putin huenda wakaingiwa na hofu kuwa ICC si asasi ya mzaha.

Kwa upande mwingine iwapo Kony ataponyoka basi Netanyahu na Putin pamoja na viongozi wengine wa ulimwenguni hawatachukulia ICC kama mahakama ambayo ina meno ya kung’ata.

Kony ni kiongozi wa waasi wa Lord’s Resistance Army (LRA) na ICC ilitoa hati ya kukamatwa kwake mnamo 2005.

ICC inalenga kumshtaki kwa makosa 39 ya kushiriki uhalifu wa kivita na kutenda makosa ya uhalifu dhidi binadamu.

Makosa hayo ni ubakaji, mauaji, kuwaingiza watoto kwenye kundi lake la kivita, dhuluma ya ngono, ndoa za lazima na mimba ya lazima kati ya 2002 na 2005.

Mnamo 2022, afisi ya ICC ilitangaza kuwa ililenga kufufua kesi hiyo na kudhibitisha mashtaka dhidi ya Kony bila uwepo wake.

Baada ya juhudi za kumkamata Kony kugonga mwamba, majaji waliruhusu kesi hiyo isikizwe bila uwepo wa kiongozi huyo wa LRA.

Jopo la majaji watatu lina kibarua cha kuthibitisha mashtaka baada ya kusikizwa kwa kesi hiyo.

Mahakama pia iliwateua mawakili ambao wangewasilisha na kumtetea Kony baada yake kukosekana wala mawakili kujitokeza kumtetea.

LRA ilianzisha baadaye miaka ya 80 ikiwa na lengo la kuondoa uongozi wa Rais Yoweri Museveni ambao umekwepo Uganda tangu 1986.

LRA ilikashifiwa kwa kuwatesa raia wa Uganda chini ya uongozi wa Kony kwa zaidi ya miaka 20.

Kipindi hicho chote LRA ilikuwa ikishiriki vita vikali dhidi ya wanajeshi wa Uganda hasa kaskazini mwa nchi hiyo na juhudi za upatanishi zilikosa kufaulu.

ICC imekuwa ikikashifiwa na baadhi ya nchi ambazo si wanachama wake na nyingine wanachama baada ya kutoa hati au amri ya kukamatwa kwa Netanyahu.

Hii ni kutokana na kiongozi huyo kuhusishwa na uhalifu na ukiukaji wa haki za kibinadamu na mauaji ya halaiki kwenye ukanda wa Gaza.

Rais wa Amerika Donald Trump amekashifu ICC kwa kutoa hati ya kukamatwa kwa Netanyahu.

Trump alienda hatua moja zaidi na kuwawekea vikwazo vya usafiri majaji wa ICC huku akionekana kuegemea mrengo wa Israeli kwenye mzozo wa Ukanda wa Gaza.