ICC yaongezewa shinikizo kuhusu kuchunguza mauaji ya waandamanaji Tanzania
MAHAKAMA ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) imepokea ombi la kuichunguza serikali ya Tanzania kuhusu madai ya ghasia na mauaji wakati wa uchaguzi mkuu wa Oktoba.
Chama cha Wanasheria wa Madrid, pamoja na mashirika kadhaa ya kutetea haki za binadamu, yanamtaka mwendesha mashtaka wa ICC kufungua uchunguzi rasmi kuhusu kile wanachokirejelea kuwa ni shambulio la kiserikali dhidi ya raia, ikiwa ni pamoja na mauaji, kuangamiza, kutesa na kuwateka nyara watu wasio na hatia.
Ombi hilo linawasilishwa wakati ambapo serikali ya Tanzania imeahirisha sherehe za Siku ya Uhuru.
Chama cha Wanasheria wa Madrid, Taasisi ya Haki za Kibinadamu, Chama cha Wanasheria Duniani na Intelwatch vimewasilisha ombi kwa mahakama ya ICC jijini The Hague nchini Uholanzi kufungua uchunguzi rasmi kuhusu matukio yaliyotokea nchini Tanzania kabla, wakati na baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 29.
Kwa mujibu wa ombi hilo, vikosi vya usalama vya Tanzania “vimeua maelfu ya raia, kuwatishia mamia na kuwateka nyara, kutesa maelfu magerezani, kuwakandamiza kingono wafungwa, kuwatimua kwa nguvu makumi ya maelfu ya Wamasai miongoni mwa masuala mengine.”
Uchaguzi wa Tanzania uliofanyika mwishoni mwa Oktoba mwaka huu ulikumbwa na maandamano yenye vurugu, uharibifu wa mali na mamia kuuawa huku wengine wakiuguza majeraha mbalimbali.
Raia walijitokeza barabarani katika miji mbalimbali nchini humo kupinga uchaguzi ambapo Samia Suluhu Hassan alikuwa akitafuta muhula wake wa kwanza kuchaguliwa kuwa rais.
Vyombo vya usalama vya serikali viliwakandamiza waandamanaji katika kile ambacho ripoti nyingi za waangalizi zinasema kilisababisha mauaji ya mamia ya raia wa Tanzania.
Ni vitendo hivi vya kikatili ambavyo walalamikaji wanataka vichunguzwe, na pia wanaitaka ICC iangazie mwaka wa 2016 ili waliokandamizwa hapo nyuma wapate fidia.
Wakili Juan Carlos Gutierrez, anasema Rais Suluhu, kama kamanda na amri jeshi mkuu, ndiye anayewajibika kwa uhalifu huo, baada ya kutoa amri raia waliokuwa wakiandamana wakandamizwe.
Utawala wa Bi Suluhu pia unahisi shinikizo kwani Kamati ya Seneti ya Mahusiano ya Kigeni ya Amerika imetaka kufanywa kwa uchunguzi huru na wa haraka kuhusu mauaji ya raia yaliyofanywa na maafisa wa usalama nchini humo.
Wiki jana, rais huyo alisema kuwa mchakato wa kupata ufadhili hautakuwa rahisi kwani nchi hiyo ‘ilitiwa doa’ na watu ambao hakuwataja.
“Mara nyingi tunategemea nje, mikopo kutoka taasisi mbalimbali za kimataifa, benki za kimataifa, lakini yaliyotokea katika nchi yetu yameharibu jina la nchi yetu kidogo,” Samia alisema.
“Hilo linaweza kupunguza sifa yetu ya kupata mikopo hiyo kwa urahisi kama tulivyofanya katika muhula wetu wa kwanza…. kilichotokea kinaweza kuturudisha nyuma hasa kimaendeleo,” aliongeza.