Kimataifa

iPhone ni za wanawake maskini, wanaume mabwanyenye hutumia Huawei – Utafiti

November 28th, 2018 Kusoma ni dakika: 1

MASHIRIKA na PETER MBURU

UTAFITI wa hivi majuzi umetoa matokeo ya kushangaza, baada ya kubaini kuwa wengi wa watumiaji wa simu za iPhone huwa masikini, huku mabwenyenye wakisemekana kupendelea simu za Huawei.

Utafiti huo wa kampuni moja kutoka China kwa jina MobData ulifanywa miongoni mwa watumiaji wa simu za kidijitali nchini China.

Ripoti yake ilisema kuwa watumiaji wengi wa simu za iPhone ni wale wa mapato ya chini na wa kawaida ambao walitajwa kuwa “watu masikini wanaotaka kujionyesha kuwa wenye pesa.”

Vilevile, utafiti ulisema kuwa wengi wa watu wanaopendelea simu za iPhone ni wanawake wasio na wapenzi wa kati ya umri wa miaka 18 na 34, ambao mapato yao ni ya chini na pia walio na elimu ya kiwango cha chini ikilinganishwa na watumiaji wa aina nyingine za simu.

Utafiti huo aidha ulidhihirisha kuwa watumiaji wa simu za Apple hawana hulka ya kuhamahama kununua aina nyingine za simu, ukisema kuwa asilimia 65.7 ya watumiaji wa simu hizo watanunua aina hiyo tu wakati wanapoamua kununua simu mpya.

Watumiaji wa Huawei nao walisemekana kuwa wanaume walio katika ndoa na kati ya umri wa miaka 25 na 34. Wengi wao wanapata mshahara mnono wakilinganishwa na wale wanaotumia iPhone na ni wafanyakazi wa taaluma Fulani ama kazi zisizo za taaluma.

Vilevile, utafiti ulisema wengi wao ni wafanyabiashara waliofanikiwa maishani.