Kimataifa

Iran yasitisha ushirikiano na mamlaka ya atomiki ikiendelea kukuza zana zake za nyuklia

Na REUTERS July 11th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

TEHRAN, IRAN

IRAN jana ilisema kuwa haitashirikiana na Mamlaka ya Kimataifa ya Atomiki (IAEA) inapoendelea na kukuza nyuklia yake, ikisema asasi hiyo sasa inadhibitiwa na kutumiwa na Amerika kuikandamiza.

Rais wa Iran Masoud Pezeshkian amesema hawataki kushirikiana na asasi hiyo waliyosema sasa inatumika kulinda maslahi ya Amerika na washirika wake.

Wiki iliyopita Pezeshkian alitia saini sheria ambayo ilisitisha ushirikiano wa Iran na IAEA, na mamlaka hiyo ikathibitisha wamewaondoa wakaguzi wake Iran.

Wakaguzi wa IAEA hutathmini kiwango ambacho nyuklia hutengenezwa ili kuhakikisha haifiki kiwango hatari chenye maangamizi.

Mara nyingi wakaguzi hawa huhakikisha taifa linalotengeneza nuklia hafikii kiwango cha kuwa na mabomu ya atomiki.

Uhusiano kati ya Iran na IAEA umesambaratika tangu Amerika na Israel zishambulie vituo vya kuunda nuklia jijini Tehran mwezi uliopita. Israel na Amerika zilitekeleza mashambulizi hayo kuzuia Iran kutengeneza mabomu ya atomiki.

Hata hivyo, Iran imekuwa ikisema kuwa nuklia yake ni kwa sababu ya amani wala hawana nia ya kuwa na bomu hatari la atomiki.

Uhusiano wetu utaendelea tu na IAEA iwapo mamlaka hiyo itabadilika na kukoma kutumika na Amerika kuharibu juhudi zetu za kutengeneza mabomu ya nuklia,” akasema Pezeshkian.

“Iwapo Iran itavamiwa tena tutakabili hali hiyo kwa njia nyingine hatari zaidi na watakaofanya hivyo watujitia kitendo chao,” akaongeza.

Iran imekuwa ikikashifu IAEA kwa kushindwa kukemea hatua ya Israel na Amerika kushambuliwa kwa nchi hiyo kuhusu nuklia.

Pia ilishangaa kwa nini mamlaka hiyo ilitoa mapendekezo ya kuonyesha Iran ilikuwa imekiuka mwongozo wa kuwa na nuklia salama bila kuwasilisha malalamishi hayo kwa Tehran.

Kushambuliwa kwa vituo vya nuklia vya Iran wakati wa vita hivyo vya siku 12 kulifanywa kupitia urushaji wa makombora na matumizi ya ndege zisizokuwa na rubani.

Wakuzi wa IAEA bado hawajafanikiwa kukagua vituo vya nuklia vilivyoharibiwa Iran japo mkuu wa mamlaka hiyo Rafael Grossi amekuwa akisema hilo ndilo lengo lake la kwanza.