Israel yaanza kuandaa mwongozo wa kuondoa Wapalestina Gaza ili kupisha Amerika
JERUSALEM, ISRAEL
WAZIRI wa Ulinzi wa Israel, Katz Alhamisi aliamrisha majeshi ya Israel yaandae mwongozo wa kupisha wakazi wa Gaza kuondoka kwenye ukanda huo baada ya Amerika kusema ingependa kuutwaa.
Rais Donald Trump kwenye mkutano na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu mnamo Jumatano, alisema kuwa Amerika ingependa kuchukua usimamizi wa Gaza ili kustawisha ukanda hao.
Kwenye kauli yake, Rais Trump aliashiria kuwa raia wa Gaza wataondolewa kwenye ardhi yao kuishi mataifa mengine kama Misri na Jordan.
Rais Trump alisema analenga kuhakikisha Gaza inang’aa na kuwa nyota ya Ukanda wa Mashariki ya Kati.
“Ninakaribisha mpango wa Rais Trump na Wapalestina wanastahili kuruhusiwa waondoke Gaza na waende mataifa mengine, jambo ambalo ni kawaida ulimwenguni,” akasema Katz.
Alipoulizwa kuhusu nani atawapokea Wapalestina, Katz alisema ni nchi ambazo zimekuwa zikipinga operesheni za kijeshi ambazo zimekuwa zikiendelezwa na Israel ukanda huo kumaliza Hamas.
“Nchi kama Uhispania, Ireland, Norway na nyingine ambazo zimekuwa zikieneza habari za uongo kuhusu vitendo vyetu Gaza, zinastahili kuwapokea Wapalestina bila kulalamika,” akaongeza.
“Unafiki wao utaanikwa wakikosa kufanya hivyo. Kuna nchi kama Canada ambazo zina mfumo wa kuwapokea wahamiaji na hapo awali imeonyesha nia ya kuwapokea wanaoishi Gaza,” akasema.
Kauli ya Rais Trump imezua joto katika ukanda wa Mashariki ya Kati na inajiri wakati ambapo Israel na Hamas zinapanga kuandaa mkumbo wa pili wa mazungumzo kumaliza vita ambavyo vimedumu Gaza kwa miezi 16.
Katz alisema mpango wa kuwaruhusu Wapalestina waondoke Gaza utahusisha wao kuvuka mipaka hadi mataifa mengine kwa miguu, kutumia uchukuzi wa majini na angani mradi mpango na mchakato wote umekamilishwa.
Urusi, China, Uingereza, Ujerumani, Jordan na Iran ni kati ya mataifa makubwa ambayo yamepinga pendekezo la Rais Trump.
Saudi Arabia ambayo ni taifa lenye uchumi mkubwa zaidi Mashariki ya Kati pia imepinga juhudi zozote za kuwaondoa Wapalestina kwenye ardhi yao.
Iran kupitia wizara yake ya Masuala ya Kigeni jana ilisema kuwa Rais Trump anashirikiana na Israel kuhakikisha kuwa Wapalestina wanaondoka Gaza au kuwamaliza kabisa kupitia vita ili Israel ichukue usukani mwa ukanda huo.