Kimataifa

Israel yajibu shambulio la Iran kama ilivyoapa licha cha kuombwa isilipize kisasi

April 19th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA MASHIRIKA

JERUSALEM, ISRAEL

HATA baada ya serikali za nchi kadhaa duniani kuiomba Israel isilipize kisasi, jeshi la nchi hiyo limekaidi wito huo na kuishambulia Iran kwa makombora.

Haya yanajiri siku chache tu baada ya Mkuu wa Jeshi la Israel Herzi Halevi kuapa kujibu shambulio lililotekelezwa na Iran siku ya Jumapili.

“Hiki kitendo cha kurushwa kwa makombora mengi na droni ndani ya himaya ya Israel kitajibiwa kwa nguvu kali zaidi,” Herzi alisema siku mbili zilizopita.

Sauti ya makombora ilisikika katika mji wa Isfahan katikati mwa Iran.

Hata hivyo, inasemakana kwamba shambulio hilo halikuleta uharibifu kubwa katika nchi hiyo.

Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki umethibitisha kwenye mitandao ya kijamii kwamba hakuna uharibifu wowote kwenye maeneo yaliyogongwa na makombora.

Wakati huo huo, Waziri mwenye msimamo mkali wa Usalama wa Taifa wa Israel, Itamar Ben-Gvir, aliandika kwenye mtandao wa kijamii wa X, kwamba shambulio la hivi karibuni la Israel dhidi ya Iran lilikuwa “dhaifu” na mdogo mno.

Safari za ndege za kibiashara zinaendelea ndani na nje ya Israeli, na mfumo wa Kamanda wa Nyumbani nchini humo, ambao una jukumu la kutoa tahadhari za vitisho kwa raia wakati wa mvutano wa kijeshi, haukutoa tahadhari yoyote.

Nchini Iran, safari za ndege zilisitishwa kwa muda asubuhi, lakini mambo yakanyooka tena saa chache baadaye.

Amerika na washirika wengine wa nchi za magharibi wamekuwa wakiitaka Israel isitishe mashambulio yake ya kijeshi ili kuepusha mzozo wa kikanda unaotokana na vita vya Israel na Hamas.

Iran ilishambulia Israel Jumamosi kujibu shambulio lililotekelezwa na Israel katika ubalozi wake jijini Damascus nchini Syria mnamo Aprili 1 mwaka huu.

Ingawa shambulio la Iran halikusababisha vifo, baada ya wanajeshi wa Israeli na washirika wake kudungua makombora hayo, limeibua hofu ya kuenea kwa vita vinavyoendelea Gaza. Aidha, kuna wasiwasi kwamba huenda vita kamili vikazuka kati ya Israel na hasidi wake wa muda mrefu Iran.

Tangu vita vilipoanza Gaza Oktoba mwaka jana, mapigano yametokea katika ya Israel na makundi washirika wa Iran, yaliyoko Lebanon, Syria, Yemen and Iraq.

Mapema Jumatatu nchi za bara Uropa, ambazo ni washirika wa Israel, ziliihimiza kujizuia na kutotekeleza mashambulio ya kulipiza kisasi Iran.

Nchini hizo; Uingereza, Ufaransa, Ujerumani ziliendeleza miito iliyotolewa na Amerika pamoja na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN) Antonio Guterres ya kuwataka viongozi wa Israel kujiepusha na hatua hiyo itakayozidisha mapigano katika eneo la Mashariki mwa Kati.