Israel Yaponda Rafah, vifaru vikivamia Gaza
VIKOSI vya Israeli vilishambulia maeneo ya katikati mwa Ukanda wa Gaza usiku kucha, na kuua watu watatu na kujeruhi mamia, huku vifaru vikizidisha uvamizi katika Rafah Kusini, madaktari na wakazi walisema.
Ndege za Israel ziliponda nyumba katika kambi ya Al-Nuseirat na kuua watu wawili na kujeruhi wengine 12, huku vifaru vikishambulia kambi ya Al-Maghazi na Al-Bureij na kujeruhi watu wengine wengi, maafisa wa afya walisema. Nuseirat, Maghazi, na Bureij ni kambi tatu kati ya nane za kihistoria za wakimbizi za Gaza.
Deir al-Balah, mji uliojaa watu waliokimbia makazi yao katikati mwa Ukanda wa Gaza, shambulio la anga la Israel lilimuua Mpalestina mmoja na kuwajeruhi wengine kadhaa siku ya Alhamisi, Juni 20, 2024, madaktari walisema.
Jeshi la Israel lilisema Jumatano kwamba vikosi vilikuwa vikiendelea na operesheni katika eneo hilo kuwalenga wanamgambo katika kile ilichokitaja kama shughuli “sahihi na za kijasusi”.
Zaidi ya miezi minane tangu vita vianze huko Gaza, Israeli sasa inalenga maeneo mawili ya mwisho ambayo vikosi vyake bado havijavamia: Rafah kwenye ukingo wa Kusini mwa Gaza na eneo linalozunguka Deir al-Balah katikati. Operesheni hizo zimelazimisha zaidi ya watu milioni moja kutoroka tangu Mei, wengi wao tayari wamehama kutoka sehemu zingine za eneo hilo.
Huko Rafah, karibu na mpaka na Misri, vifaru vya Israel viliingia ndani kabisa katika maeneo ya Magharibi na katikati mwa mji huo vikiongeza mashambulizi ya mabomu, na kulazimu familia zaidi zinazoishi katika maeneo ya Pwani kukimbilia kaskazini.
Baadhi ya wakazi walisema kasi ya uvamizi huo imeongezwa katika siku mbili zilizopita.
“Vifaru vilidhibiti maeneo mengi ya Rafah. Watu wanaoishi kando ya ufuo pia wameanza kuondoka kuelekea Khan Younis na maeneo ya kati kwa hofu kwa sababu ya kuendelea kwa mashambulizi ya mabomu,” alisema Abu Wasim, mkazi kutoka kitongoji cha Al-Shaboura cha Rafah, ambaye aliacha nyumba yake zaidi ya wiki moja iliyopita kabla ya vifaru kuingia katikati mwa jiji.
Rafah ilihifadhi zaidi ya nusu ya watu milioni 2.3 wa Gaza hadi Mei 7 wakati vikosi vya Israeli vilipoanza kushambulia mji huo.
Hakujawa na dalili ya kusitisha mapigano huku juhudi za wapatanishi wa kimataifa wakiungwa mkono na Amerika zikishindwa kushawishi Israel na Hamas kukubaliana kukomesha mapigano.
Mnamo Alhamisi, Israel iliwaachilia Wapalestina 33 waliokuwa wamezuiliwa miezi kadhaa iliyopita na wanajeshi wa Israel katika maeneo tofauti ya eneo hilo.
Wafungwa walioachiliwa wamelazwa katika Hospitali ya Al-Aqsa huko Deir Al-Balah katikati mwa Ukanda wa Gaza baada ya kulalamikia kuteswa na kudhulumiwa na vikosi vya Israel.