Israel yatangaza kumuua msemaji wa Hamas Abu Obeida huko Gaza
MSEMAJI wa kitengo cha kivita cha Hamas Abu Obeida ameuawa katika shambulio la angani jijini Gaza City, Ukanda wa Gaza, Israel imesema.
Waziri wa Ulinzi wa Israel Israel Katz, kupitia taarifa katika jukwaa la X, Jumapili alipongeza Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF) kwa kufanikisha mauaji hayo.
Hakutoa maelezo zaidi kuhusu wakati au mahala ambapo operesheni hiyo ilitekelezwa.
Hata hivyo, awali, IDF ilisema ndege yake ilishambulia “gaidi mkuu” katika makazi ya Rimal Jumamosi. Hapo ndipo vyombo vya habari nchini Israel vilianza kutoa habari kwamba Obeida ndiye aliuawa.
Hamas, hata hivyo, haijathibitisha kuuawa kwa msemaji huyo.
Awali, kundi hilo la Kipalestina lilisema raia kadhaa waliuawa na wengine wakajeruhiwa kufuatia mashambulio yaliyotekelezwa na Israel katika jumba moja la makazi katika kitongoji hicho.
Kwenye taarifa yake Jumapili Waziri Katz alionya kuwa washirika wengine wa Obeida watalengwa katika operesheni itakayoendelezwa Gaza.
Obeida ni miongoni mwa wakuu wachache wa kitengo cha kivita cha Hamas waliosalia, na waliokuwepo, kundi hilo lilipotekeleza msururu wa mashambulio Kusini mwa Israel Oktoba 7, 2023.
Israel inasema kuwa Obeida alihudumu kama “uso wa kundi la kigaidi la Hamas na alisambaza propaganda za Hamas”.
Aidha, kwa muda mrefu Obeida, anayeaminika kuwa na umri wa miaka 40, alitoa shutuma kali dhidi ya Israel kwa niaba ya tawi la kivita la Hamas, “al-Qassam Brigades.”