Israel yavamia Al Jazeera baada ya amri ya kufungwa kwa kituo chake cha runinga
Na MASHIRIKA
JERUSALEM, Israel
MAAFISA wa Israel walivamia chumba kimoja cha hoteli jijini Jerusalem kinachotumiwa na shirika la habari la Al Jazeera kama afisi baada ya serikali kuamua kufunga runinga ya shirika hilo Jumapili.
Shirika hilo la habari linamilikiwa na taifa la Qatar, linaloendesha mazungumzo ya kupatanisha Israel na Hamas. Viongozi wakuu wa kundi hilo linalotawala Ukanda wa Gaza, pia wanaishi Qatar.
Kwenye video iliyosambazwa mitandaoni, maafisa waliovalia mavazi ya kiraia walionekana wakibomoa mitambo ya kamera katika hoteli hiyo, duru za Al Jazeera zilisema iko mashariki mwa Jerusalem.
Amri ya kufungwa kwa kituo hicho ilitolewa na baraza la mawaziri wa Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu likidai kuwa shirika hilo ni tishio kwa usalama wa kitaifa wa Isreal.
Lakini shirika la Al Jazeera lilitaja hatua hiyo kama “kitendo cha uhalifu”.
Aidha, lilitaja tuhuma kwamba kituo hicho kinatishia usalama wa kitaifa wa Israel kama “hatari na uwongo wa kimzaha” unaweka wanahabari wake hatarini.
Al Jazeera imesema itafuata mkondo wa kisheria katika jitihada zake za kutaka hatua hiyo, ya kuzima kituo chake, ibatilishwe.
Shirika hilo la habari limekosoa operesheni za wanajeshi wa Israel katika Ukanda wa Gaza, katika taarifa zake kuhusu vita hivyo tangu Oktoba mwaka jana.
“Kituo cha Al Jazeera kinachoendeleza uchochezi kitafungwa nchini Israel,” Netanyahu akasema kwenye taarifa fupi kupitia mtandao wa kijamii baada ya barabara la mawaziri kufikia uamuzi huo kwa kauli moja.
Taarifa moja ya serikali ilisema kuwa Waziri wa Mawasiliano wa Israel alitia saini agizo la kufanikisha utekelezaji wa uamuzi huo.
Kulingana na taarifa hiyo, iliamuliwa kuwa afisi ya Al Jazeera nchini Israel zifungwe, izuiwe kupata mawimbi ya mawasiliano kutoka kwa kampuni za satilaiti na tovuti yake ifungwe. Haikutaja shughuli za shirika hilo katika ukanda wa Gaza.
Kufuatia uamuzi huo wa serikali ya Israel, kampuni za kutoa huduma za mawasiliano na satilaiti nchini Israel zilisitisha matangazo ya Al Jazeera.
Serikali ya Qatar inayomiliki shirika hilo la habari, haikutoa kauli yoyote rasmi kujibu kuzimwa kwa Al Jazeera nchini Israel.
Mwezi jana, shirika hilo la habari lililalamikia kile kilichotaja kama “mashambulio ya kila mara dhidi yetu bila sababu maalum” na Israel.
Al Jazeera ilisema Israel ililenga, kimakusudi, na kuua wanahabari wake kadhaa, wakiwemo Samer Abu Daqqa na Hamza AlDahdooh.
Wawili hao waliuawa wakati wa vita katika Ukanda wa Gaza.
Lakini Israel imeshikilia kuwa huwa hailengi wanahabari.
Serikali ya Qatar ilianzisha shirika la habari la Al Jazeera mnamo 1996 na hulitumia kujenga hadhi na sifa zake ulimwenguni.
“Shirika la Habari la Al Jazeera linalaani vikali kitendo hiki cha uhalifu kinachokiuka haki za kibinadamu na haki ya kimsingi ya walimwengu kupata habari,” shirika hilo lilisema kwenye taarifa.
“Al Jazeera inadumisha haki yake na kuendelea kupeperusha habari na taarifa kwa hadhira yake ulimwenguni,” likaongeza.
Shirika la Umoja wa Mataifa kuhusu Haki za Kibinadamu pia lilikosoa hatua ya Israel kufunga kituo cha habari cha Al Jazeera jijini Jerusalem.
“Tunasikitishwa na uamuzi wa mawaziri kuzima Al Jazeera nchini Israel,” shirika hilo la haki likasema kupitia akaunti yake ya mtandao wa X.