Kimataifa

Jamii za wafugaji Kenya, Uganda zashauriana namna ya kugawana nyasi

January 26th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

OSCAR KAKAI Na LABAAN SHABAAN

VIONGOZI wa jamii ya Wapokot walioenda kuomba waruhusiwe kulisha mifugo yao nchini Uganda wamefukuzwa.

Kundi la wazee 12, mabalozi wa amani, maafisa wa usalama na viongozi kutoka Kaunti ya Pokot Magharibi walifunga safari kuenda wilaya ya Kween, Uganda.

Wakiongozwa na Naibu Gavana Robert Komolle, walielekea Uganda kufanya mazungumzo ili kuomba nyasi na maji.

“Tumekuja kwa amani na sisi wote ni wa jamii ya Wakalenjin. Tutafuata makubaliano ili tuweze kulisha mifugo yetu ambayo imeathiriwa na kiangazi,” akasema Bw Komolle.

Naye Mzee Joseph Lopetang’ole akanyenyekea: “Tumekuja kuwaomba nyasi na maji.”

Kulingana na watu wa eneo la Sebei, ilikuwa ni kejeli kwa viongozi wa jamii ya Pokot kuomba ruhusa ya kulisha mifugo ilhali wachungaji kutoka wilaya ya Amudat na kaunti ya Pokot Magharibi tayari walikuwa wameingia kwenye maeneo ya malisho.

Kiangazi kimekausha malisho na chemchemi za maji maeneo ya Pokot Magharibi lakini upande huo mwingine wa Uganda, inapokaa jamii ya Wasebei, majani ni mabichi na kuna maji.

Kulikuwa na malumbano kati ya makundi hayo mawili huku wakazi wa Sebei, wakuu wa utawala na viongozi wakiondoka kwenye mkutano huo.

Makundi hayo mawili yalikosa kuelewana kuhusu kulisha mifugo katika eneo hilo. Juhudi za maridhiano zinaendelea.

Wakuu wa utawala na wakazi wa eneo la Sebei waliwasuta wachungaji kwa kuharibu mazao yao mashambani, kuvamia mashamba na kuiba mifugo.

Wachungaji mifugo walifurushwa kutoka Uganda mwaka 2023 baada ya mauaji mengi na wizi wa mifugo kuripotiwa nchini humo.

Juhudi za upatanisho zinaendelea huku viongozi kutoka jamii ambazo zimeathiriwa wakiratibu mkutano mwingine leo Ijumaa.