Jaribio la mapinduzi DRC lilihusisha raia 3 wa Amerika, Jeshi lasema
KINSHASA, DRC
ALIYEKUWA kiongozi wa watu waliojaribu kupindua serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) Jumapili ameuawa na takriban watu 50 wakiwemo raia watatu wa Marekani kukamatwa, msemaji wa jeshi nchini DRC aliliambia shirika la Reuters.
Milio ya risasi ilisikika mwendo wa saa kumi za usiku katika mji mkuu Kinshasa, ripota wa Reuters alisema.
Watu waliojihami kwa silaha walishambulia ofisi ya Rais Felix Tshisekedi katikati mwa jiji, kulingana na msemaji Sylvain Ekenge.
Aidha, shambulio lingine lilitokea katika nyumba ya, mbunge Vital Kamerhe, ambaye anatarajiwa kuwa spika, msemaji wa Kamerhe, Michel Moto Muhima, na balozi wa Japan alisema kwenye kwenye mtandao wa X (awali Twitter).
Katika tukio hilo, Moto Muhima alisema walinzi wawili na mshambuliaji mmoja waliuawa katika tukio hilo.
Kombora lililorushwa kutoka Kinshasa lilipiga jiji la Brazzaville katika nchi jirani ya Jamhuri ya Congo, na kuwajeruhi watu kadhaa, serikali ya nchi hiyo ilisema katika taarifa yake, na kuongeza kuwa mtu mmoja amelazwa hospitalini akiuguza majeraha.
Ekenge alimtaja Christian Malanga, mwanasiasa wa Congo ambaye huishi Amerika, kuwa mshukiwa mkuu aliyeongoza jaribio la kuipindua serikali.
“Malanga alishindwa kwa kumalizwa nguvu kabisa wakati wa shambulio la Palais de la Nation, Aboubacar fulani alitengwa wakati wa shambulio nyumbani kwa Vital Kamarhe [na] wengine – karibu 50 wakiwemo raia watatu wa Amerika – walikamatwa na kwa sasa wanahojiwa na Vikosi vya Wanajeshi vinavyotoa huduma maalumu,” Ekenge aliambia Reuters.
Alisema Malanga alijaribu kwa mara ya kwanza kuipundua serikali mwaka 2017 lakini akashindwa na kwamba mmoja wa raia wa Amerika waliokamatwa ni mtoto wa Malanga.
Ukurasa katika mtandao wa Facebook unaoonekana kuwa wa Malanga ulichapisha video ya moja kwa moja ya kile kinachoonekana kuwa shambulio hilo.
“Sisi, wanamgambo, tumechoka. Hatuwezi kuendelea na Tshisekedi na Kamerhe, wamefanya mambo mengi ya kijinga katika nchi hii,” Malanga alisema kwa lugha ya Lingala kwenye video hiyo, ambayo haijathibitishwa na Reuters.
Balozi wa Amerika, Lucy Tamlyn alisema katika chapisho kwenye mtandao wa kijamii kuwa “anatiwa wasiwasi sana” na ripoti kwamba raia wa Amerika walidaiwa kuhusika katika matukio hayo.
“Tafadhali tunawahakikishia kwamba tutashirikiana na serikali ya DRC kwa kiwango kamili wanapochunguza vitendo hivi vya uhalifu na kuchukulia hatua kali raia yeyote wa Amerika anayehusika na vitendo vya uhalifu,” alisema.