Jela baada ya kuripoti kuwa alinajisiwa
MASHIRIKA Na PETER MBURU
MWANAMUME amehukumiwa kifungo cha miezi minane gerezani nchini Tunisia, baada ya kuripoti kwa polisi kuwa wezi wawili wanaume waliofika nyumbani kwake walimwibia kisha wakamlawiti kwa nguvu.
Mwanamume huyo wa miaka 22 anasemekana kuwa alienda katika kituo cha polisi kusini mwa taifa hilo, mji wa Sfax kuripoti visa hivyo viwili; cha kuibiwa na kulawitiwa, lakini akaishia kukamatwa.
Alifungwa kulingana na sheria za nchi hiyo ambazo zimeharamisha mapenzi ya jinsia moja, ijapokuwa alibakwa.
Kikundi fulani cha kutetea haki za wanaume mashoga kilisema mwanamume huyo alilaumiwa kuwa alishiriki ngono na wanaume wenzake na akalazimishwa kufanyiwa ukaguzi katika njia ya choo.
Korti iliamrisha mwanamume huyo ahudumu kifungo cha miezi minane jela kwa kushiriki ngono na wanaume na kusingizia watu baada ya kuamua kuwa alifanya mapenzi na wanaume hao kwa hiari, ripoti kutoka Tunisia zikasema.
Wanaume aliodai walimlawiti nao walitupwa jela miezi minane kwa kushiriki ngono ya jinsia moja, kumuumiza mtu na wizi.
Kikundi cha wanaharakati cha Shams kilisema familia ya mwanamume huyo iliachwa ikishangaa baada ya uamuzi huo wa korti. Wameamua kukata rufaa ya uamuzi huo.
Wanaharakati hao wameanzisha kampeni kwenye mitandao kusukuma mwanamume huyo aachiliwe.
Mnamo Novemba, kikundi cha wanaharakati kilidai kuwa wanaume wanaoshukiwa kushiriki mapenzi ya jinsia moja Tunisia wanalazimishwa kufanyiwa ukaguzi wa njia ya choo.
“Madaktari wanaingiza wadhulumiwa kidole ama kitu kingine kwenye njia ya choo kupima ikiwa huwa wanashiriki ngono ya jinsia moja. Hii si mbinu ya kisayansi, inakiuka sheria za kimataifa na inaweza kuwaadhiri watu wanaokaguliwa kwa namna hiyo. Ni hatari zaidi kwa wanaolawitiwa,” likasema shirika moja lisilo la serikali.
Shirika hilo liliitaka Tunisia kulinda haki za binadamu na kukoma kuwapitishia raia wake mateso ya aina hiyo.
Kulingana na sheria ya Tunisia, watu wanaopatikana na hatia ya kushiriki mapenzi ya jinsia moja hufungwa hadi miaka mitatu gerezani.