Jela miaka 20 kwa kuua mumewe na kutia mwili kwa mitungi ya maji
MASHIRIKA Na PETER MBURU
MWANAMKE ambaye alimuua mumewe kisha akamkatakata na kuweka sehemu za mwili wake ndani ya mitungi ya maji katika nyumba yao nchini Marekani amefungwa jela miaka 20.
Bi Marcia Eubank wa miaka 50 kutoka eneo la Coventry Twonship alikiri mbele ya korti kuwa aliua mumewe kwa kutumia silaha, kisha akaharibuharibu maiti yake, katika kisa kilichotambulika Desemba 21, 2018.
Wachunguzi walieleza korti kuwa Marcia alimpiga risasi mumewe Howard Eubank wa miaka 54 kichwani mnamo Juni 13, 2017 kisha akakatakata mwili wake na kuhifadhi sehemu hizo ndani ya mitungi.
Mwanamke huyo alikiri Desemba 2018, miezi sita baada ya kisa kutendeka, wakati mtoto wao wa kiume alishtuka kukumbana na jaa la taka lililokuwa na baadhi ya sehemu za mwili wa babake.
Mtoto huyo alikuwa amesahau funguo za nyumba mnamo Desemba 9 na hivyo akaamua kupitia dirishani kuingia, wakati aliona kreti ambayo ilikuwa imewekelewa tupa na wadudu na akaamua kulifungua.
Alimtumia mamake ujumbe mfupi kwa simu, na akakiri kuwa alimuua mumewe.
Mwanamke huyo alikamatwa siku hiyo. Wanawe walisema kuwa alidanganya kila mtu kuwa alimtaliki na akahamia eneo la Texas.
“Sote tuliona kuwa haikuwa kawaida kuwa aliamka siku moja tu na kuamua kuondoka lakini hatukuwahi kudhani kuwa angekuwa alimuua,” akasema Jonathon, mwanawe marehemu.
Mvulana huyo alisema kuwa walikuwa wamezungumza na babake mwezi kabla ya kisa hicho kuhusu harusi yake ya Agosti mwaka huo, lakini akashangaa kupokea ujumbe mnamo Juni kuwa alikuwa ameondoka hata bila kufahamisha watu.
Alisema miezi kadha iliyofuata, akaunti ya Facebook ya babake ilikuwa ikichapishwa jumbe ‘akisema kuwa alikuwa salama huko Texas’. Ni baada ya mambo kufahamika tu ambapo alifahamu kuwa jumbe hizo zilikuwa zikichapishwa na mamake.
Wakili wa Marcia alieleza korti kuwa mwanamke huyo aliteswa na mumewe kiakili na kwa kuchapwa, walipokuwa katika ndoa yao ya miaka 25.
Lakini familia ilieleza korti kuwa ni mwanamke huyo ambaye alikuwa na hulka ya kumtusi mumewe, japo marehemu hakuwahi kumchapa.