Kimataifa

Jeshi la Sudan lakomboa mji wa Obeid huku waasi wa RSF wakiunda serikali Nairobi

Na MASHIRIKA February 25th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

CAIRO, MISRI

JESHI la Sudan Jumapili lilikomboa mji wa Obeid na kurejesha shughuli za uchukuzi katika eneo la kusini mwa nchi hiyo baada ya vita vya miaka miwili kati yake na kundi la wapiganaji la Rapid Support Force (RSF).

Wanajeshi hao pia waliweza kuwafurusha wapiganaji wa RSF kutoka ngome yake ya mwisho ya mkoa wa White Nile, msemaji wa jeshi Brigedia Jeneral Nabil Abdullahi alisema kwenye taarifa Jumapili.

Haya yalijiri huku RSF wakikongamana Nairobi kuunda kile walichotaja kuwa muungano wa ‘Sudan Founding Alliance’ waliosema ni mwanzo wa hatua ya kuunda serikali ya umoja katika taifa hilo lililozongwa na vita.

Hatua hiyo inaonekana kama pigo jingine kwa kundi hilo la wapiganaji ambalo limekuwa likiendeleza vita na jeshi la Sudan tangu Aprili mwaka jana.

Mapigano hayo, ambayo yameathiri pakubwa jiji kuu Khartoum, na miji mingine yameshuhudia maovu kama vile ubakaji, mauaji ya kikabila, uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya kibinadamu haswa eneo la magharibi la Darfur.

Hii ni kulingana na Umoja wa Mataifa na makundi ya kimataifa ya kutetea haki.