Jesus alivyosaidia Arsenal kubomoa Palace Carabao Cup
KOCHA Mikel Arteta amemiminia sifa Gabriel Jesus baada ya Mbrazil huyo kuzamisha Crystal Palace 3-2 kwenye robo-fainali ya kipute cha Carabao Cup, Jumatano usiku.
Jesus, ambaye amekosolewa vikali na mashabiki – baadhi yao wakitaka auzwe kwa kupoteza nafasi tele za kufunga bao – alionyesha makali yake kwa kumwaga kipa Dean Henderson dakika ya 54, 73 na 81.
Hii ilikuwa baada ya Jean-Philippe Mateta kuweka Palace mbele dakika ya nne.
Bao la Jesus la kwanza na mwisho lilipatikana kupitia asisti ya nahodha Martin Odegaard naye Bukayo Saka akachangia asisti nyingine.
Mchezaji wa zamani wa Arsenal, Eddie Nketiah, alifungia Palace goli la pili dakika ya 85.
“Nimefurahishwa na kazi ya Jesus. Alikuwa na ukame wa muda mrefu bila bao na leo amepata matatu kwa mpigo. Alionekana ngangari sana leo,” alitanguliza kocha Arteta.
“Nadhani ni kitu cha maana sana kwake na pia timu kwamba tunaweza kutegemea mchezaji mwenye ukatili kama huu. Anatoa mchango muhimu. Gabi ni mtu muhimu sana kwetu,” akaeleza Mhispania huyo.
Jesus hakuwa ameona lango katika mechi nane tangu achangie bao moja, wanabunduki wa Arsenal wakizamisha Preston North End 3-0 mnamo Oktoba 30 kwenye mechi ya kujikatia tiketi ya robo-fainali.
Bao hilo ndilo pekee alikuwa amepata tangu Arsenal ianze msimu Agosti 17.
“Inafurahisha sana kupata mabao matatu leo. Nashukuru Martin Odegaard na Bukayo Saka kumega pasi murwa nilizofunga,” alideka Jesus.
Katika robo-fainali nyingine, Darwin Nunez na Harvey Elliott walifungia Liverpool ikipepeta Southampton 2-1 ugani St Mary’s, Cameron Archer akipachika bao la Saints kufutia chozi.
Newcastle nao walichabanga Brentford 3-1 kupitia mabao ya Sandro Tonali (mawili) na Fabian Schar, huku Yoane Wissa akafariji timu yake ya Brentford na goli katika dakika za lala-salama ugani St James’ Park.
Robo-fainali ya mwisho kati ya Tottenham Hotsput na Manchester United iliratibiwa kuchezwa jana usiku. Kisha droo ya nusu-fainali itafuata mara moja baada ya mchuano huo.