Jiji kuu nchini Indonesia kuhamishwa
Na MASHIRIKA na MARY WANGARI
JAKARTA, Indonesia
RAIS wa Indonesia Joko Widodo, alitangaza Jumatatu kwamba jiji kuu nchini humo litahamishwa kutoka eneo lenye msongamano, linalozama na lenye uchafuzi wa mazingira la Jakarta, hadi eneo lenye idadi ndogo ya watu Kalimantan Mashariki katika kisiwa cha Borneo kinachofahamika kwa misitu na nyani aina ya orangutans.
Rais Widodo alisema utafiti wa kina katika kipindi cha zaidi ya miaka mitatu iliyopita uliishia katika uteuzi wa eneo hilo katika upande wa mashariki mwa kisiwa cha Borneo.
“Hatungeendelea kuruhusu mzigo katika Jakarta na kisiwa cha Java kuongezeka kuhusiana na idadi ya watu. Tofauti za kiuchumi kati ya Java na kwingineko zitaongezeka vilevile,” alisema Widodo, kwenye mkutano na wanahabari katika ikulu ya Rais.
Katika mkutano na wanahabari mnamo Julai 2019, Rais huyo alisema anataka kutenganisha kituo kikuu cha serikali kutoka kwa kituo kikuu cha biashara na uchumi jijini Jakarta.
Jakarta ni mfano wa jiji kuu la bara Asia lenye watu kati ya milioni 10 na 30 ikiwemo watu walio katika eneo kuu lake.
Huwa linakumbwa mara kwa mara na mitetemeko ya ardhi na mafuriko na linazama kwa haraka kutokana na uchimbaji wa maji ardhini.
Maji ya kemikali
Maji yanayochimbwa ardhini yameathiriwa pakubwa na kemikali ikiwemo mito yake.
Imekadiriwa kwamba msongamano hugharimu uchumi wa taifa hilo Sh6.7bilioni kila mwaka.
Eneo lenye utajiri wa madini la Kalimantan Mashariki liliwahi wakati mmoja kufunikwa kabisa na misitu ya mvua, lakini ukataji miti haramu umeondoa kiasi kikubwa cha mimea yake asilia.
Linasheheni watu 3.5 milioni pekee na linazingirwa na Mbuga ya Kitaifa ya Wanyamapori ya Kutai inayofahamika kwa nyani wa asili ya orangutans, aina nyingine ya kima na wanyamapori.