Kimataifa

Jinsi majimbo saba muhimu yalivyompa Trump ushindi kirahisi

Na MASHIRIKA November 6th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

WASHINGTON DC, AMERIKA

RAIS wa zamani wa Amerika Donald Trump alijizolea asilimia kubwa ya kura kutoka majimbo saba yaliyokuwa na ushindani mkubwa kati yake na mpinzani wake Kamala Harris.

Taarifa kutoka vituo mbalimbali vya habari zinaonyesha kuwa Trump alijizolea kura nyingi sana kutoka jimbo la Pennsylvania.

Kando na hayo, Trump pia alishinda katika majimbo muhimu ya Georgia na North Carolina.

Kwa ujumla, Trump ameshinda majimbo mengi zaidi, ikiwa ni pamoja na Texas na Ohio yenye kura nyingi katika uchaguzi.

Naye mpinzani wake mkuu Kamala Harris alipata kura nyingi katika eneo la kaskazini mashariki na jimbo lake la nyumbani la California.

Hii ilimsukuma Trump mbele na kumpa ushindi mkubwa katika uchaguzi huo ambao umekuwa ukisubiriwa kwa hamu na ulimwengu.

Huku Trump akijigamba na hata kujitokeza hadharani kuhutubia wafuasi wake kama mshindi, mpinzani wake Harris hakuzungumza na wafuasi wake, ambao walikuwa wamekusanyika katika chuo kikuu cha Howard.

Mwenyekiti mwenza wake wa kampeni, Cedric Richmond, alihutubia umati akisema Harris atazungumza hadharani siku ya Jumatano.

“Bado tuna kura zinazoendelea kuhesabiwa,” Richmond aliambia wanahabari.

Rais huyo wa zamani alikuwa akionyesha nguvu katika maeneo mengi ya nchi, akitangaza na kuboresha utendaji wake wa 2020 kila mahali kuanzia maeneo ya mashambani hadi mijini.

Wanarepublican walishinda viti vingi katika seneti vilivyokuwa vikishikiliwa na Democratic katika majimbo ya West Virginia na Ohio.

Hakuna chama chochote kilichoonekana kuwa na nguvu katika vita vya kuwania udhibiti wa Bunge la Wawakilishi ambapo Wanarepublican kwa sasa wanashikilia uongozi lakini mwembamba sana.

“Tunaongoza seneti na inaonekana tutafanya hivyo katika Bunge la Wawakilishi,” Trump aliambia wafuasi wake akiwalimbikizia sifa tele kwa kusimama naye wakati wa kampeni na wakati wa kura.

Trump alipata uungwaji mkono zaidi kutoka kwa Wahispania, wapiga kura wa jadi wa chama cha Democratic, na familia za kipato cha chini ambazo zimehisi kufinywa na kupanda kwa bei tangu uchaguzi uliopita wa rais wa 2020, kulingana na kura za maoni kutoka shirika la Edison.

Trump alishinda asilimia 45 ya wapiga kura wa Uhispania kote nchini, akimfuata Harris kwa asilimia 53.

Takriban asilimia 31 ya wapiga kura walisema uchumi ndio suala lao kuu, na walimpigia kura Trump kwa asilimia 79, kulingana na kura za maoni.

Asilimia 45 ya wapiga kura kote nchini walisema hali ya kifedha ya familia zao ilikuwa mbaya zaidi leo kuliko miaka minne iliyopita, na walimpendelea Trump.

Imetafsiriwa na WINNIE ONYANDO