Kimataifa

Kasisi asimamishwa kazi kwa kumzaba kofi mtoto

June 25th, 2018 Kusoma ni dakika: 1

Na MASHIRIKA na VALENTINE OBARA  

PARIS, UFARANSA

KASISI wa Kanisa Katoliki amesimamishwa kazi kwa kumzaba kofi mtoto mchanga aliyekuwa akilia wakati akimbatiza.

Kasisi Jacque Lacroix, 89, wa Dayosisi ya Meaux, Ufaransa, alionekana kwenye video akijaribu kumnyamazisha mtoto huyo aliyebebwa na mamake, lakini mtoto alipoendelea kulia akamzaba kofi.

Video hiyo iliyosambazwa mitandaoni iliibua hisia kali katika mitandao ya kijamii ndipo wakuu wa dayosisi hiyo wakaamua kuchukua hatua.

Taarifa ya dayosisi hiyo iliyochapishwa na mashirika ya habari ilisema kasisi huyo sasa amepigwa marufuku kuongoza shughuli za ubatizo na harusi.

Alipohojiwa na wanahabari, Kasisi Lacroix alijitetea kwamba hakutumia nguvu na kile kilichoonekana kuwa kofi kilikuwa ni kumpapasa tu mtoto shavuni.

“Mtoto alikuwa Analia sana na nilihitaji kumgeuza kichwa ili nimimine maji. Nilikuwa namwambia anyamaze lakini akakataa. Nilichofanya kilikuwa katikati ya kumpapasa na kofi kidogo tu. Nilikuwa najaribu kumnyamazisha, sikujua cha kufanya,” akasema.

Katika video hiyo, baba mtoto ambaye alikuwa amesimama nyuma ya mama aliyembeba alisonga mbele kwa haraka mtoto wake alipochapwa kofi kicha akamchukua kwa lazima huku kasisi akionekana kutaka kumbatiza kwa lazima huku mtoto akizidi kulia.