• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 6:39 PM
Kenya, Haiti zaivisha dili ya polisi 1,000 kupelekwa kukabili magenge

Kenya, Haiti zaivisha dili ya polisi 1,000 kupelekwa kukabili magenge

NA MWANDISHI WETU

KENYA na Haiti zimetia saini makubaliano ya mkataba wa polisi 1,000 kutumwa katika taifa hilo la Carribean linalokabiliwa na mzozo wa kisiasa huku magenge ya uhalifu yakiteka nyara rasilimali muhimu za nchi.

Rais William Ruto na Waziri Mkuu wa Haiti Ariel Henry wameshuhudia utiaji saini wa makubaliano hayo mnamo Ijumaa katika Ikulu ya Nairobi.

Waziri Mkuu Henry alitua nchini baada ya kuhudhuria mkutano muhimu wa 46 wa marais na viongozi wa serikali wa mataifa wanachama wa jumuiya ya Carribean (CARICOM) lililoandaliwa Guyana mnamo Jumatano.

Katikati ya Februari, Inspekta Mkuu Walter Nyankieya Nyamato aliaga dunia ndani ya hoteli moja jijini Washington DC, Marekani. Polisi huyo alikuwa sehemu ya timu ya awali iliyotumwa nchini Haiti.

Mnamo Januari 26, 2024, serikali ya Kenya ilikuwa imepata pigo kubwa ilipozimwa na mahakama kupeleka polisi 1,000 nchini Haiti.

Jaji Enock Mwita alisema Baraza la Kitaifa la Usalama (NSC) halina mamlaka yoyote kuwapeleka polisi nchini Haiti.

Jaji Mwita alisema uamuzi wa Rais Ruto na wanachama wa baraza la NSC kuwapeleka maafisa wa polisi Haiti ilikinzana na Kifungu nambari 240(8) cha Katiba ya Kenya.

Kwa mujibu wa kifungu hicho, polisi hawastahili kupelekwa nchi za ng’ambo kudumisha amani. Jukumu la kudumisha amani mataifa ya kigeni ni la wanajeshi.

Alisema sheria inaeleza kwamba maafisa wa Jeshi wanajumuisha Jeshi la Nchi Kavu, Jeshi la Angani (Airforce) na Jeshi la Wanamaji (Navy).

“Baraza la NSC halina mamlaka yoyote kuamuru maafisa wa polisi 1,000 kupelekwa nchini Haiti kupambana na magaidi wanaohatarisha maisha ya wananchi kule. Polisi si wanajeshi. Sheria inakitambua kikosi cha polisi kuwa cha kutoa huduma tu kwa wananchi humu nchini,” alisema Jaji Mwita.

Jaji huyo alisema ijapokuwa Rais Ruto aliahidi Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa (UNSC) kufanya hivyo, sheria za nchi hazitambui idara ya polisi kama “kikosi cha wajeshi kilicho na uwezo kupelekwa kudumisha amani ng’ambo.”

Jaji huyo alisema polisi wameruhusiwa tu kudumisha usalama nchini na wala sio nje.

Ijapokuwa kaulimbiu ya polisi wa Kenya ni ‘Utumishi kwa Wote’, Jaji Mwita alisema “huduma za polisi zinafaa kutolewa humu nchini tu na si katika mataifa ya ng’ambo.”

Alisema Kenya na Haiti hazina mkataba wowote wa kubadilishana hudumu za kiusalama na hivyo basi polisi wa Kenya hawawezi kuhudumu Haiti.

Jaji huyo alisema iwapo kuna dharura humu nchini, baraza la usalama hutoa mwelekeo wa kuwapeleka maafisa wa polisi katika eneo husika na “mamlaka ya NSC hufika hapo tu.”

Hata wakati maafisa wa Jeshi wanapopelekwa nje, Baraza la Mawaziri hukutana na kupitisha idadi itakayoenda kisha hoja huwasilishwa bungeni waende.

Baada ya bunge kuidhinisha wanajeshi waende, ndipo mkuu wa vikosi vya majeshi nchini (KDF) huteua maafisa watakaosafiri kisha wanapewa bendera ya Kenya kupeperusha nchini wanamoenda kudumisha amani.

Jaji Mwita alisema ijapokuwa Waziri wa Usalama wa Ndani Prof Kithure Kindiki alipeleka suala la maafisa hao 1,000 wa polisi kuenda Haiti kujadiliwa bungeni, hatua hiyo inakinzana na sheria.

“Baada ya kutathmini ushahidi wote uliowasilishwa mbele yangu, nimefikia uamuzi kwamba hatua ya NSC kupeleka polisi 1,000 Haiti inakinzana na Kifungu nambari 240 (8) cha Katiba. Polisi wa Kenya hawatapelekwa Haiti. Itakuwa ni kinyume cha sheria,” akasema jaji Mwita wakati huo.

  • Tags

You can share this post!

Wakulima wa ndizi Taita Taveta watafutiwa soko kimataifa

Ishara ya ‘ngono’ uwanjani yamletea noma Ronaldo nchini...

T L