Kimataifa

Kinara wa upinzani aikosoa serikali kwa kumhangaisha

September 23rd, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na AFP

ADDIS ABABA, Ethiopia

KIONGOZI wa upinzani nchini Ethiopia, Jawar Mohammed ameambia mahakama kwamba, anajivunia kufunguliwa mashtaka ya ugaidi.

Jawar ambaye ana ushawishi mkubwa nchini humo hakukiri mashtaka hayo. Badala yake, alilaumu serikali kwa kulenga viongozi wa upinzani kama yeye.

Jawar alishtakiwa pamoja na watu wengine 22 na shirika moja la habari.

Mashtaka dhidi yao yanahusiana na wimbi la ghasia za kikabila zilizozuka kufuatia mauaji ya mwanamuziki Hachalu Hundessa mnamo Juni.

Watu zaidi ya 150 walifariki kwenye ghasia hizo baada ya mwanamuziki huyo kutoka jamii ya Oromo anakotoka Jawar kuuawa kwa kupigwa risasi jijini Addis Ababa.

Jawar, watu hao 22 na shirika la habari la Oromia Media Network (OMN) ambalo alikuwa akisimamia wanalaumiwa kwa kuhusika na ugaidi, kupatikana na silaha na kukiuka sheria za mawasiliano.

Maelezo ya mashtaka hayo hayakutolewa lakini inadaiwa walichochea ghasia hizo.

Hii ilikuwa mara ya kwanza kwa Jawar kufikishwa kortini tangu mashtaka yalipofichuliwa Jumamosi. Jawar amekuwa akizuiliwa tangu Juni 30.

Akiwa amevalia suti alipofikishwa kortini Addis Ababa, Jawar alionekana mchovu.

Hata hivyo alipoanza kuzungumza, alikuwa na nguvu na ujasiri wake kawaida.

“Najivunia kwa kushtakiwa kwa ugaidi kwa mara ya pili katika maisha yangu,” aliambia mahakama.

Aliwahi kushtakiwa kwa mashtaka sawa na hayo alipokuwa akiishi uhamishoni Amerika kutokana na uhusiano wake na OMN lakini mashtaka hayo yaliondolewa wakati waziri mkuu, Abiy Ahmed alipoingia mamlakani Aprili 2018.

Akiwa kortini, Jawar alilaumu serikali kwa kukamata na kuzuilia yeyote anayeshukiwa kuwa mpinzani kwenye uchaguzi mkuu ujao. Alisema serikali imetambua kwamba chama chake cha Oromo Federalist Congress, kilikuwa maarufu kuliko chama tawala cha Prosperity Party.

Uchaguzi ulikuwa umepangwa kufanyika Agosti lakini ukahamishwa kwa sababu ya janga la corona.

Mwanasiasa huyo ambaye alikuwa mshirika wa Abiy amemlaumu waziri huyo mkuu na mshindi wa tuzo la amani la Nobel kwa kukosa kushughulikia malalamishi ya muda mrefu ya jamii ya Oromo. Wote wawili wanatoka jamii hiyo kubwa nchini Ethiopia.

Lakini Abiy anasema kwamba, watu wanaopinga mageuzi anayofanya wamekuwa wakitumia mbegu ya uhasama wa kijamii na kidini.