Kiongozi wa genge Haiti aagiza wakongwe 110 kuuawa ‘kwa kumroga mwanawe akafa’
PORT-AU-PRINCE, HAITI
WATU 110 waliuawa mwishoni mwa wiki katika kitongoji cha Cite Soleil nchini Haiti baada ya kiongozi wa genge la wahalifu kuamuru wakongwe washambuliwe akidai walisababisha kifo cha mwanawe kupitia uchawi, Shirika la Kitaifa la Kutetea Haki za Binadamu (RNDDH) lilisema Jumapili.
Shirika hilo lilisema wote hao waliouawa walikuwa wenye umri wa zaidi ya miaka 60.
Monel “Mikano” Felix kiongozi wa genge la Wharf Jeremie aliamuru mauaji hayo baada ya mwanawe kuugua, RNDDH ilieleza.
Inasemekana Felix alishauriwa na mganga mmoja kwamba watu wakongwe eneo hilo ndio walimdhuru mtoto huyo kupitia uchawi.
Wanachama wa genge hilo waliuwa watu 60 Ijumaa na wengine 50 Jumapili wakitumia mapanga na visu, kwa mujibu wa RNDDH.
Cite Soleil, kitongoji chenye watu wengi karibu na bandari ya jiji kuu Port-au-Prince, ni miongoni mwa makazi duni ambayo wakazi wake ni masikini zaidi.
Aidha, ni miongoni mwa makazi nchini Haiti ambako visa vya utovu wa usalama vimekithiri mno.
Genge la wahalifu limedhibiti makazi hayo na kiasi cha kuzuia wakazi kutumia simu za mkononi. Hii imefanya wengi kukosa kusambaza habari kuhusu mauaji hayo.
Mnamo 2022, Felix – akiwa kiongozi wa genge la Wharf Jeremie – alipigwa marufuku kuingia nchi jirani ya Jamhuri ya Dominica.
Kulingana na RNDDH, mwanawe Felix alifariki Jumamosi jioni.
Hapo mwezi Oktoba, Shirika la Umoja wa Mataifa (UN) lilikadiria kuwa idadi ya wanachama wa genge la Felix ilikuwa imefika 300, na kwamba wanaendesha shughuli zao karibu na maeneo ya Fort Dimanche na La Saline.
Mnamo Novemba 2018 raia 71 waliuawa eneo la La Salin huku mamia ya nyumba zikiteketezwa katika ghasia zilizozuka.
Jimmy “Barbecue” Cherizier, ambaye ni kiongozi wa muungano wa magenge kwa jina Viv Ansanm ambao huendesha shughuli zake maeneo kadhaa ya Port-au-Prince, aliwekewa vikwazo na UN.
Anatuhumiwa kupanga mauaji ya La Saline wakati bado alikuwa akihudumu kama afisa wa polisi, miongoni mwa uhalifu mwingine.
Mwezi Oktoba mwaka huu, watu 115 waliuawa kinyama katika mji wa Pont-Sonde ulioko eneo la Artibonite kunakokuzwa chakula kwa wingi nchini Haiti.
Genge la Gran Grif lilisema mauaji hayo yalikuwa ya kulipiza kisasa hatua ya wakazi kushirikiana na kundi moja la usalama, kuwazuia kukusanya pesa barabarani.
Serikali ya Haiti, ambayo inalemazwa na mivutano ya kisiasa, inajitahidi kudhibiti ongezeko la magenge yenye silaha ndani na nje ya jiji kuu Port-au-Prince.
Mnamo 2022 utawala uliomba usaidizi wa walinda usalama wa mataifa ya kigeni kusaidiana na polisi wa nchi hiyo kupambana na magenge hayo.
Ombi hilo liliidhinishwa na Baraza la Usalama la UN (UNSC) mnamo 2023, lakini kufikia sasa ni taifa la Kenya pekee limetuma polisi 400 nchini humo.