Kiongozi wa mapinduzi ya kijeshi nchini Guinea ashinda urais
CONAKRY, Guinea
KIONGOZI wa mapinduzi ya kijeshi nchini Guinea, Mamady Doumbouya, ametangazwa mshindi wa uchaguzi wa urais, hatua inayokamilisha mpito wa kurejea utawala wa kiraia katika taifa hilo lenye utajiri mkubwa wa madini.
Tume ya uchaguzi ilisema Doumbouya alipata asilimia 86.72 ya kura katika uchaguzi uliofanyika Desemba 28.
Mahakama ya Juu ina siku nane kuthibitisha matokeo hayo.
Doumbouya, aliyekuwa kamanda wa kikosi maalum cha jeshi alichukua mamlaka mwaka 2021 baada ya kumuondoa madarakani Rais wa wakati huo Alpha Condé, aliyekuwa amehudumu tangu 2010.
Mapinduzi hayo yalikuwa miongoni mwa msururu wa mapinduzi tisa yaliyotikisa Afrika Magharibi na Kati tangu 2020.
Viongozi wakuu wa upinzani, akiwemo Condé na kiongozi mkongwe Cellou Dalein Diallo, wako uhamishoni, hali iliyomwacha Doumbouya akikabiliana na wagombea wanane tu.
Hapo awali, katiba ya mpito baada ya mapinduzi iliwazuia wanajeshi wa junta kuwania uchaguzi. Hata hivyo, katiba mpya iliondoa vikwazo hivyo kupitia kura ya maoni ya Septemba.
Akitoa tangazo la matokeo, mwenyekiti wa tume ya uchaguzi Djenabou Touré alisema asilimia 80.95 ya wapiga kura walijitokeza.
Hata hivyo, ushiriki ulionekana mdogo katika mji mkuu Conakry, huku wanasiasa wa upinzani wakipinga takwimu hizo kama ilivyokuwa kwenye kura ya maoni ya Septemba.
Guinea ina utajiri mkubwa wa bauxite duniani na Simandou, mradi uliozinduliwa rasmi mwezi uliopita.
Doumbouya amejinasibu kuharakisha mradi huo na kuhakikisha nchi inanufaika na rasilimali zake.
Serikali yake pia ilibatilisha leseni ya kampuni tanzu ya Emirates Global Aluminium, Guinea Alumina Corporation, kutokana na mgogoro wa kusafisha madini, na kuhamisha mali zake kwa kampuni ya serikali.
Mwelekeo huo, unaoonekana pia Mali, Burkina Faso na Niger, umeongeza umaarufu wake.