Kitovu cha ghasia? Amerika yaonya raia wake kuhusu vurugu za maandamano mapya Tanzania
AMERIKA jana ilitoa tahadhari ya kiusalama kwa raia wake wanaoishi Tanzania, ikionya kuwa kuna uwezekano wa ghasia kutokea wakati wa maandamano dhidi ya serikali yatakayofanyika Desemba 9.
Ubalozi wa Amerika nchini Tanzania umeonya kuwa maandamano hayo yanaweza kuanza mapema Desemba 5 na kuwataka raia wake hasa wale wanaosafiri kuwa makini na kuchukua tahadhari.
Kwa mujibu wa tahadhari hiyo, ghasia zilizoshuhudiwa wakati na baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 29 zilichangia kuharibiwa kwa miundomsingi, kuzimwa kwa intaneti na kuvurugika kwa shughuli za uchukuzi, visa ambavyo vinaweza kutokea siku zijazo.
Ubalozi huo ulionya kuwa wanaosafiri Tanzania wiki zinazokuja wanastahili kujiandaa kwa safari zao kuvurugika, uwezekano wa kuwepo kwa kafyu, kuzimwa kwa intaneti, kusitishwa kwa uchukuzi wa feri hadi Zanzibar na kusitishwa kwa safari za ndege za kuingia na kutoka Tanzania.
Iliongeza kuwa raia wa kigeni ambao wapo Tanzania sasa wanafuatiliwa kwa makini sana na vyombo vya usalama nchini humo.
Ubalozi huo uliwaambia raia wa Amerika kuwa kuwasaidia kutakuwa ngumu iwapo ghasia na maandamano yataenea.
Iliwaomba raia wajiepushe kuwa kwenye maeneo ambayo kuna mikusanyiko ya watu, waandae vyakula vya ziada na pia wazingatie kafyu iwapo itatangazwa.
Tanzania tayari imefuta maadhimisho ya Siku ya Uhuru mnamo Disemba 9, hatua hiyo ikikisiwa inatokana maandamano yanayopangwa dhidi ya serikali.