Kimataifa

Kujiuzulu kwa Spika Kamerhe kwatikisa Bunge la DR Congo

Na MASHIRIKA September 25th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

KUJIUZULU kwa spika wa bunge la kitaifa la Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, Vital Kamerhe kumezua mdahalo kuhusu uhusiano wake na Rais wa nchi hiyo Felix Tshisekedi.

Tangazo la Kamerhe liliwashangaza wabunge, wengi wao wakiwa na shauku ya kumwajibisha kwa kile walichokitaja kuwa ni uzembe kazini.

Katika hotuba yake ya kujiuzulu, Kamerhe aliongeza mabadiliko mengine: nia yake ya “kuendelea kutumikia taifa la Congo pamoja na Rais Félix Tshisekedi.”

Vital Kamerhe (kushoto) akiwa na Rais Felix Tshisekedi awali. Wachanganuzi wasema uhusiano wao umeingia mdudu. Picha|Reuters

Wachambuzi walikuwa wamegusia kuhusu tofauti kati wawili hao, iliyochochewa na dhamira zao za ushindani za kisiasa.

“Sichochewi na hasira au chuki dhidi ya mtu yeyote. Moyo wangu ni mdogo sana kuweza kulemewa na mambo kama hayo,” alisema.

Lakini matamshi yake pia yalibeba maonyo ya siri.

Wakati huo huo, Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron, amesema nchi yake itaandaa mkutano wa dharura kuangazia ukosefu wa misaada ya kibinadamu katika nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Oktoba.

Akizungumza Jumanne katika Umoja wa Mataifa, Macron alisema kuna haja ya kurejesha matumaini ya wakazi wa Kivu na maelfu ya watu ambao wamelazimika kuyakimbia makazi yao.

Baada ya mazungumzo ya miezi mitatu nchini Qatar, waasi wa M23 na serikali ya Congo waliazimia kusitisha mapigano baada ya kusaini makubaliano Julai 19, kufuatia makubaliano mengine ya amani yaliyosainiwa mjini Washington kati ya serikali ya Congo na Rwanda mwishoni mwa mwezi Juni.