Lesotho yathibitisha kisa cha kwanza cha Covid-19
Na MASHIRIKA
MASERU, Lesotho
LESOTHO, taifa la kipekee barani Afrika ambalo halikuwa limeripoti maambukizi ya virusi vya corona Jumatano lilitangaza kuwa limegundua kisa cha kwanza cha Covid-19.
Virusi vinavyosababisha ugonjwa huo vilipatikana katika mtu mmoja miongoni mwa watu 81 ambao sampuli zao zilifanyiwa vipimo baada ya kuwasili nchini humo wiki jana kutoka Saudi Arabia na taifa jirani la Afrika Kusini, Wizara ya Afya ilisema kwenye taarifa.
“Wizara ya Afya ingependa kuwaarifu raia wa Lesotho kwamba taifa sasa limethibitisha kisa cha kwanza cha Covid-19,” Mkurugenzi wa Afya Dkt Nyane Letsi alisema.
Mgonjwa huyo ni raia wa Lesotho anayesomea nchini Saudi Arabia.
Kuthibitishwa kwa kisa hicho cha maambukizi sasa kunaashiria kuwa mataifa yote 54 ya bara la Afrika yameathiriwa na changamoto hii ya kiafya.