Kimataifa

Maandamano dhidi ya ubaguzi Afrika Kusini yafanyika Amerika

September 25th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na MASHIRIKA

NEW YORK, Amerika

MAMIA ya raia wa Afrika Kusini walikusanyika mjini New York mnamo Jumamosi kuonyesha umoja wao katika kupinga ubaguzi wa Waafrika nchini Afrika Kusini.

Maandamano hayo matulivu yalishuhudia raia wa Afrika Kusini wapatao 200 kutoka New Jersey, Maryland, California, Colorado, Washington, Massachusetts na Pennsylvania wakikusanyika Times Square, New York, kwa maandamano ya kimyakimya.

Maandamano hayo yaliandaliwa na mwanaharakati wa ubadilishanaji utamaduni Afrika Kusini, Iman Jeneker, aliyesema kwamba aliposikia habari hizo kutoka Afrika Kusini alihisi kufa ganzi.

“Nilihisi kutengwa kutoka kwa dada zangu. Nisingeweza kuwepo hapo kusimama pamoja nao na kufanya sauti yangu isikike na kuomboleza na kila mmoja,”

Jeneker alijitosa katika mtandao wa kijamii wa Facebook kuwarai raia wote wa Afrika Kusini kuunga mkono juhudi hizo za kupinga ubaguzi.

Ujumbe wake ulivutia wengi na punde alipata kibali kutoka kwa Idara ya Polisi New York.

“Najivunia kwamba tuna ujasiri wa kufanya hivi lakini pia nahofia kuwa sauti zetu hazitoshi,”

“Rais wetu ametoa ahadi na tunamsihi azitimize. Wanawake wanataka tu kujihisi salama, tunataka tu kujua kina dada zetu, mama na binti zetu kule nyumbani wanaweza kuenda afisini pasipo kubakwa na kuuawa,” alisema Jeneker.

Mitandao ya kijamii

Akizungumza na wanahabari, msanii wa maelezo ya filamu, aliyetengeneza video ya maandamano hayo, Lyla Illing, alisema kuwa alisoma kuhusu janga hilo kwenye mitandao ya kijamii.

“Katika wiki ya kwanza Septemba na hasa habari zilipozuka kuhusu Uyinene, nilishindwa kuenda kuingia katika mitandao ya kijamii pasipo kumbi zangu kujazwa na visa kuhusu dhuluma za kijinsia, ubaguzi wa rangi na mauaji kule nyumbani,” alisema Illing.

“Nilihisi kana kwamba hakuna jingine ila habari za kuvunja moyo kwenye mtandao wangu. Hakukuwa na njia ya kupuuza. Raia wa Afrika Kusini walikuwa wakitangaza kwa sauti kwamba hili lilikuwa tatizo kuu,”

“Wakati wa maandamano hayo ya kimya kimya, tulichukua dakika 10 kutengeneza mviringo ambapo wanawake walizungumza, wakisoma mashairi au kuomba. Wengi wetu tulilia wakati huu huku wanawake wakikumbatiana ili kutiana moyo.”

Illing alisema kwamba anatumai maandamano hayo yatawafaidi wanawake Afrika Kusini.