Maandamano ya Gen Z yamlazimu Waziri Mkuu wa Nepal kujiuzulu
HATIMAYE Waziri Mkuu wa Nepal KP Sharma Oli amejiuzulu baada ya kulemewa na presha za vijana wa Gen Z walioandamana kwa siku kadhaa kupinga ufisadi na kuzimwa kwa mitandao ya kijamii nchini humo.
Msaidizi wake alithibitisha kuwa Rais Ram Chandra Paudel amekubali kujiuzulu kwa Oli hatua ambayo imelitumbukiza taifa katika hali ya ati ati kisiasa.
Watu 19 wamekufa na zaidi ya wengine 100 kujeruhiwa katika fujo hizo mbaya zaidi kuwahi kutokea nchini humo.
Mnamo Jumatatu, maandamano hayo yalifikia kilele pale baadhi ya waandamanaji walipokaidi kafyu na wakavamia majengo ya bunge jijini Kathmandu na kuteketeza magari ikiwemo ambulansi.
Serikali ililazimika kuondoa marufuku iliyoweka dhidi ya matumizi ya jumla ya mitandao 26 ya kijamii.
Huku wakipambana na polisi, waliowakabili kwa vitoa machozi na risasi za mipira, waandamanaji waliteketeza nyumba kadhaa za viongozi wa nchi hiyo.
Nyumba hizo ni pamoja na za Kiongozi wa chama cha Nepalii Congress Sher Bahadur Deube, Rais Ram Chandra Poudel, Waziri wa Masuala ya Ndani Ramesh Lekhak na Waziri Mkuu wa zamani Pushpa Kamal Dahal.
Uwanja mkuu wa Ndege jijini Kathmandu pia ulifungwa hadi muda usiojulikana.
Awali, Jumanne, Oli aliongoza mkutano wa vyama vya kisiasa akihimiza kufanyika kwa mazungumzo kurejesha utulivu “kwa masilahi ya taifa.”
Wito wake haukuzingatiwa huku hamaki za wananchi zikiendelea kupanda na kukaidi vikosi vya usalama.
Nchi ndogo ya Nepal iliyoko kati ya India na China, imezongwa na misukosuko ya kisiasa na changamoto za kiuchumi baada kuondolewa kwa utawala wa kifalme, kupitia maandamano ya umma, mnamo 2008.
IMETAFSIRIWA NA CHARLES WASONGA