• Nairobi
  • Last Updated June 15th, 2024 1:54 PM
Maangamizi ya halaiki yananukia Sudan, UN yaonya

Maangamizi ya halaiki yananukia Sudan, UN yaonya

NEW YORK, AMERIKA

MSHAURI maalum wa Umoja wa Mataifa (UN) kuhusu kuzuiwa kwa mauaji ya halaiki ameonya kuhusu hatari ya kutokea kwa uhalifu huo nchini humo na kwamba huenda tayari vitendo hivyo vinatekelezwa.

“Raia nchini Sudan wanafaa kulindwa haraka,” Alice Nderitu akasema.

“Ipo hatari ya kutokea kwa mauaji ya halaiki Sudan. Ni kweli na hatari hiyo inaendelea kushuhudiwa, kila siku.” akaongeza.

Bi Nderitu alisema hayo Jumanne alipohutubia mkutano wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa (UNSC) kuadhimisha miaka 25 tangu kupitishwa kwa uamuzi kuhusu kulindwa kwa raia katika mapigano.

Mkutano huo pia ulitumiwa kuadhimisha miaka 75 tangu kutiwa saini kuhusu Mikataba ya Geneva kuhusu udumishaji wa haki za raia wakati wa vita.

Bi Nderitu alisema raia wengi wa Sudan wanalengwa nyakati za vita kwa misingi ya asili yao.

“Katika maeneo ya Darfur El Fasher, raia wanashambuliwa na kuuawa kwa sababu ya rangi ya ngozi yao, kwa sababu ya kabila lao, kwa sababu ya utambulisho wao,” Nderitu akasema kwenye hotuba iliyopeperushwa kwa njia ya video.

“Vile vile, wanalengwa na matamshi ya uchochezi na yanaweza kusababisha vita,” akaongeza.

El Fasher ni mji mkuu katika eneo la Kaskazini mwa Darfur, ambako juzi mapigano yalitokota kati na wanajeshi wa Sudan (SAF) waliojita kambi humo na wapiganaji wa kundi la waasi la RSF wanaoripotiwa kukaribia mji huo kwa lengo la kuuteka.

Mji wa El Fasher ni wa kipekee katika eneo la Darfur ambao haujatekwa na RSF.

Zaidi ya raia 800,000 wanaishi mjini humo na mapigano huenda yakachangia kutoka kwa maovu yanayofanana na yale ya mauaji ya halaiki yaliyotekelezwa na wapiganaji wa Janjaweed dhidi ya makabila ya Zaghawa, Masalit, Fur na mengineyo mapema miaka ya 2,000.

Wanachama wa kundi la Janjaweed, la asili ya Kiarabu, ndio walijigeuza kuwa wanachama wa RSF.

“Mashambulio yaliyochochewa kikabila yakilenga jamii za Masalit, Fur na Zaghawa, yamekuwa yakiripotiwa na yanaendelea kuripotiwa. Kimsingi, yanatekelezwa na RSF na makundi ya wapiganaji ya asili ya Kiarabu,” Nderitu akaeleza.

“Wanaripotiwa kutekeleza mashambulio kwa mtindo fulani ambapo wanalenga maeneo na watu fulani. Hii ni ishara kuwa wanaendelea nia au lengo fulani,” akaongeza.

Lengo la kuua na kuharibu ni sehemu ya uhalifu wa mauaji ya halaiki.

Bi Nderitu alisema mashamubulio yaliyoripotiwa katika vijiji viungani mwa mji wa El Fasher yanaonekana kulenga kufurusha watu kutoka makwao na kusababisha hofu, badala ya kufikia malengo fulani ya kijeshi.

“Ni muhimu kwamba hatua za kuwalinda raia wasio na hatia mjini El Fasher na kote nchini Sudan, zichukuliwe,” akasema.

  • Tags

You can share this post!

Gachagua aomba Uhuru waungane

Mkenya Cheruiyot Kirui alielewa kibarua cha kuukwea Mlima...

T L