Kimataifa

Maelfu ya waandamana Amerika kupinga sera za Trump na Elon Musk

Na REUTERS, BENSON MATHEKA April 6th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

MAELFU ya waandamanaji Jumamosi walikusanyika Washington, D.C., na sehemu mbalimbali za Amerika, kama sehemu ya maandamano dhidi ya Rais Donald Trump na mshirika wake bilionea Elon Musk tangu walipoanzisha juhudi za kufanyia serikali mageuzi na kupanua mamlaka ya urais.

Watu walimiminika kwenye eneo linalozunguka Mnara wa Washington chini ya anga la mawingu na mvua nyepesi. Waandalizi waliambia Reuters kuwa watu zaidi ya 20,000 walitarajiwa kuhudhuria mkutano huo katika National Mall.

Takriban makundi 150 ya wanaharakati yalijiandikisha kushiriki, kulingana na tovuti ya tukio hilo. Maandamano yalipangwa katika majimbo yote 50 pamoja na Canada na Mexico.

Terry Klein, mwanasayansi mstaafu kutoka Princeton, New Jersey, alikuwa miongoni mwa waliokusanyika karibu na jukwaa chini ya Mnara wa Washington. Alisema alishiriki maandamano kupinga sera za Trump kuhusu “kila kitu kuanzia uhamiaji hadi suala la DOGE, ushuru wa forodha hadi elimu. Namaanisha, nchi yetu yote iko chini ya mashambulizi, taasisi zetu zote, kila kitu kinachoifanya Amerika kuwa Amerika.”

Watu waliendelea kuongezeka karibu na mnara huo siku nzima. Baadhi walibeba bendera za Ukraine, wengine walivaa shuka za Kipalestina (keffiyeh) na kubeba mabango yenye maandishi “ komboa Palestina,” huku wabunge kutoka chama cha Democratic wakilaani sera za Trump jukwaani.

Wayne Hoffman, mwenye umri wa miaka 73, msimamizi wa fedha mstaafu kutoka West Cape May, New Jersey, alisema alikuwa na wasiwasi kuhusu sera za kiuchumi za Trump, hasa matumizi ya ushuru wa forodha.
“Wakulima katika wataumia. Watu watapoteza kazi – hasa akiba zao za uzeeni. Watu wamepoteza makumi ya maelfu ya dola,” alisema Hoffman.

Kyle, kijana wa miaka 20 kutoka Ohio anayefanya mafunzo ya kazi alikuwa mfuasi pekee wa Trump kwenye maandamano hayo, akiwa amevaa kofia yenye maandishi “Make America Great Again” na kutembea pembezoni mwa mkutano huo akijadilina na waandamanaji.
“Watu wengi si wakali sana. Wachache wanafoka matusi,” alisema Kyle, ambaye alikataa kutaja jina lake la mwisho.

Trump, ambaye wiki hii alitikisa masoko ya fedha duniani na kuchochea taharuki kimataifa kwa wimbi la ushuru wa forodha, alitumia siku hiyo huko Florida, akicheza gofu katika klabu yake ya Jupiter kabla ya kurejea Mar-a-Lago alasiri.

Takriban kilomita 6 kutoka Mar-a-Lago huko West Palm Beach, waandamanaji zaidi ya 400 walikusanyika wakiwa wamevalia mavazi ya rangi nyepesi. Madereva walipiga honi kuunga mkono waandamanaji hao.
“Masoko yameporomoka, Trump anacheza gofu,” yalisema maandishi katika bango moja.

Katika maandamano mengine Stamford, Connecticut, Sue-ann Friedman, mwenye umri wa miaka 84, alibeba bango jekundu alilolitengeneza mwenyewe kupinga mipango ya serikali kupunguza ufadhili wa utafiti wa matibabu.
“Nilidhani siku zangu za  kuandamana zilikuwa zimeisha, hadi tukapata mtu kama Musk na Trump,” alisema Friedman.

Paul Kretschmann, wakili mstaafu mwenye umri wa miaka 74 huko Stamford, alisema ilikuwa mara yake ya kwanza kushiriki maandamano.
“Wasiwasi wangu ni kuwa usalama wa jamii utaporomoka, tutapoteza mafao yetu, na hakutakuwa na mtu wa kuyasimamia. Ninaogopa huu ni mpango mkubwa wa kuivunja serikali ili Trump aweze kudumu madarakani,” alisema