Mafuriko, radi, dhoruba, yahangaisha walimwengu
MAFURIKO, radi na dhoruba yanaendelea kuhangaisha walimwengu mvua kubwa ikishuhudiwa katika nchi mbalimbali.
Wengi wamelazimika kuhama makazi yao kutafuta maeneo salama huku maelfu wakiendelea kupata matibabu.
Kwa sasa, nchi kadhaa zikiwemo China, Pakistan, Rwanda, Kenya, Tanzania, Italia, Slovenia na Ugiriki zinakabiliwa na mafuriko.
Japo idadi kamili ya vifo duniani haijabainishwa, inakadiriwa kuwa mafuriko hayo yamesababisha maafa ya maelfu ya watu.
Kwa mfano, zaidi ya watu 140 wamefariki dunia nchini Pakistan baada ya kupigwa na radi na matukio mengine yanayohusishwa na dhoruba huku taifa hilo likishuhudia mvua kubwa kuliko kawaida.
Pakistan imekumbwa na mafuriko makubwa na maporomoko ya ardhi.
Mafuriko hayo yameharibu miundombinu, kuporomosha majengo na hata kuwaacha maelfu bila makazi.
Msemaji wa Idara ya Hali ya Hewa nchini humo, Zaheer Ahmad Babar, alisema taifa hilo limeshuhudia mvua kubwa zaidi.
Mnamo mwaka 2022, theluthi moja ya Pakistan ilifunikwa na maji kufuatia mvua kubwa kuwahi kushuhudiwa zilizofanya mamilioni ya watu kuhama makazi yao.
Benki ya Dunia inakadiria kuwa taifa hilo lilipata hasara ya Sh4 trilioni kutokana na mvua hizo.
Wakati uo huo, zaidi ya watu kumi wameaga dunia Rwanda kutokana na mafuriko.
Philippe Habinshuti, katibu mkuu anayesiamamia Wizara inayohusika na Usimamizi wa Dharura Jumanne aliwaambia waandishi wa habari kuwa baadhi ya waathiriwa waliuawa na maporomoko ya udongo huku wengine wakipigwa na radi.
Vifo hivyo vilitokea katika wilaya ya Rutsiro magharibi mwa Rwanda, ambapo watu wawili waliuawa na maporomoko ya ardhi kufuatia mvua kubwa iliyonyesha mapema Jumanne.
Katika tukio jingine, mama na mtoto wake walipoteza maisha katika wilaya ya Gasabo mjini Kigali baada ya nyumba yao kuporomoka wakati wa mvua.
Mvua hiyo iliyonyesha pia imesababisha uharibifu wa mali zikiwemo nyumba, mazao na miundombinu katika maeneo mbalimbali nchini humo.
Tathmini kamili ya kubaini ukubwa wa athari bado inaendelea, kulingana na wizara.
Mamlaka ya Hali ya Hewa ya Rwanda ilionya Jumatatu kwamba maeneo kadhaa ya Rwanda yataendelea kupata mvua kubwa mwezi huu.
Serikali imewataka wakazi wanaoishi katika maeneo hatari kuhamia maeneo salama.
Mei mwaka jana, mafuriko na maporomoko ya ardhi yalipiga magharibi na kaskazini mwa Rwanda, na kusababisha vifo vya watu 135.
Kwa upande mwingine, mafuriko hayo yameleta maadhara Tanzania huku mamia wakilazimika kuyahama makazi yao kutafuta maeneo salama.
Takriban watu 155 wamefariki Tanzania wiki moja iliyopita kutokana na mafuriko na maporomoko ya ardhi.
Kassim Majaliwa alitahadharisha kuwa huenda mvua itaendelea kunyesha mwezi huu na kuzitaka familia kuondoka katika maeneo yanayokumbwa na mafuriko.
Takriban watu 200,000 na zaidi ya kaya 51,000 tayari zimeathiriwa na mafuriko hayo.