Kimataifa

Mahakama ya Korea Kusini yaidhinisha kukamatwa kwa Rais Yoon

Na MASHIRIKA December 31st, 2024 Kusoma ni dakika: 2

MAHAKAMA ya Korea Kusini Jumanne iliidhinisha kibali  cha kukamatwa kwa Rais Yoon Suk Yeol, anayeandamwa na bunge,  kufuatia uamuzi wake wa kutangaza sheria ya kijeshi mnamo Desemba 3, maafisa wanaomchunguza walisema.

Ofisi ya Uchunguzi wa Ufisadi kwa Viongozi wa Vyeo vya Juu (CIO) ilithibitisha Mahakama ya Wilaya ya Seoul Magharibi iliidhinisha kibali ilivyoombwa na wachunguzi wanaochunguza hatua ya Yoon kutangaza sheria ya kijeshi kwa muda mfupi

Hiki ni kibali cha kwanza cha kukamatwa kwa rais aliye madarakani nchini Korea Kusini, kulingana na vyombo vya habari vya ndani.

Kibali cha  sasa cha kukamatwa linaweza kutumika hadi Januari 6, na mara litakapotekelezwa, Yoon anatarajiwa kuzuiliwa katika gereza jijini Seoul, shirika la habari la Yonhap lilisema likinukuu CIO.

Mahakama ilitoa  kibali hicho kutokana na uwezekano kwamba Yoon hatatii akiitwa na wachunguzi, na kukiwa na sababu kubwa ya kushuku Yoon kwa uhalifu, Yonhap ilisema. Mahakama ilikataa kutoa maoni.

Yoon amekataa wito wa wapelelezi kuhojiwa mara tatu tangu kutangazwa kwa sheria ya kijeshi  Desemba 3.

Yoon anakabiliwa na uchunguzi wa uhalifu kwa madai kuwa aliongoza maasi. Maasi ni mojawapo ya mashtaka machache ambayo rais wa Korea Kusini hana kinga.

Haikuwa wazi ni lini au vipi  kibali cha kukamatwa kwa Yoon kitatekelezwa. Idara ya usalama ya rais wa Korea Kusini ilisema katika taarifa siku ya Jumanne kwamba itashughulikia agizo la kukamatwa kwa mujibu wa taratibu zinazofaa.

Mahakama pia iliidhinisha kibali cha kupekua makazi ya Yoon, CIO ilisema.

Hapo awali, polisi walijaribu lakini walishindwa kuivamia ofisi ya rais kama sehemu ya uchunguzi, baada ya huduma ya usalama ya rais kuwazuia kuingia.

Kaimu kiongozi wa chama tawala cha People Power Party cha Korea Kusini, Kweon Seong-dong, alisema siku ya Jumanne kwamba kujaribu kumweka kizuizini rais aliye madarakani ni jambo lisilofaa.

Kim Yong-min, mbunge katika chama cha upinzani cha Democratic, ambacho kina wabunge wengi na kulichowasilisha hoja ya  kumuondoa Yoon, alisema Jumanne “mchakato wa kutekeleza kibali na uchunguzi unaweza kuwa mgumu sana,”,akitoa wito kwa wachunguzi kutekeleza mara kibali hicho.

IMETAFSIRIWA NA BENSON MATHEKA