KimataifaMakala

Mapasta wachunguzwa baada ya ‘walioponywa’ kuteta Nigeria

Na MOHAMMED MOMOH, CHARLES WASONGA September 19th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

UTAWALA nchini Nigeria umeanzisha uchunguzi kuhusu shughuli za wahubiri bandia wanaodai kuwa na kipawa cha kutibu magonjwa sugu, kufurusha mashetani na kuuza maji matakatifu.

Hii ni baada ya watu kadhaa kulalamika kuhadaiwa na baadhi ya makanisa yanayoongozwa na wahubiri hao.

Bi Angela Andrew ni mmoja wa wale waliolalamika kwa kupinga madai ya kanisa moja kuwa lilimponya dadake ambaye amepoteza uwezo wa kusikia na kuongea.

Aliweka bango la kanisa hilo katika akaunti yake ya mtandao wa Tik Tok, lililokuwa na picha ya dadake ikiambatanishwa na maelezo, “Sis Ekoma- ambaye amekuwa kiziwi na bubu kwa miaka 30 ameponywa.”

Bi Andrew alitaja madai hayo kama yasiyo ya kweli na kwamba dadake bado alikuwa hawezi kuongea wala kusikia.

Watu kadha wamewasilisha malamishi sawa na hayo dhidi ya kanisa hilo.

Kwa mfano, Adelabu Johnson, 36, alijitokeza na kudai kuwa kanisa hilo lilidai kumponya babake.

“Babake bado yuko nyumbani akiugua kiharusi. Kanisa kanisa moja lilidai katika krusedi mjini Lagos kwamba mzee huyo mwenye umri wa miaka 72 alifaa kurejeshwa nyumbani kwa sababu alikuwa ameponywa na kwamba baada ya saa sita angeamka na kuanza kutembea,” akasema.

“Sasa ni zaidi ya mwezi mmoja, babangu angali mgonjwa na tumeamua kutegemea huduma za matibabu za kisasa,” Johnson akaeleza.

Makanisa nchini Nigeria yamedai kutibu magonjwa sugu kama vile kansa, Ukimwi na hata mtu kutokuwa na uwezo wa kupata watoto.

Viongozi wa makanisa hayo hutumia mashahidi “walioponywa” ili waweze kuvutia waumini wengi.

Idadi kubwa ya waumini huwawezesha viongozi wa makanisa hayo kupata kiwango kikubwa cha sadaka na fungu la 10.

Lakini hii sio njia ya kipekee ya kusaka pesa.

Baadhi ya viongozi wa makanisa wanauza bidhaa ya “kimiujiza” kama vile, maji matakatifu, mafuta ya baraka, vitambaa vya baraka na vitafunio spesheli kwa waumini walio tayari kulipia chochote ili wapate utajiri.

Kanisa la Christ Mercyland Deliverance Ministry, liko katika mji wa Effurun katika jimbo la Delta. Kanisa hilo linaongozwa na mwinjilisti wa televisheni Jeremiah Fufeyi.

Maafisa kutoka asasi husika za serikali wameanza kuchunguza kanisa hilo na makanisa mengine ambayo hutoa madai kama hayo kwa lengo la kuvutia waumini wengi.

Maafisa wa Mamlaka ya Kitaifa ya Kusimamia Matumizi ya Chakula na Dawa (Nafdac) walimwagiza Pasta Fufeyin kufika mbele yao ili achunguzwe kuhusu madai ya kutoza ada kwa shughuli za kanisa lake.

Hii ni baada ya Nafdac kupata malalamishi mwishoni mwa Agosti 2024 kwamba kanisa  hilo liliweka vibandiko kwenye chupa za sabuni ya maji na kuyauza kama “maji ya uponyaji”.

Ilidaiwa kuwa kanisa hilo lilikuwa likiuza chupa moja kwa dola 2 za Amerika (Sh260), madai ambayo yalichochea hasira miongoni mwa wananchi.

Hata hivyo, baadhi ya waumini wameendelea kutoa shuhuda za kusifu ufaafu wa “maji matakatifu” yanayouzwa na viongozi wa makanisa husika. Wanadai ufanisi wao unatokana na maombi ya mapasta hao.

Shughuli za uponyaji magonjwa na kuwafukuza mashetani zimeshamiri zaidi katika makanisa ya Kipentekosti.

Makanisa haya ni pomoja na Synagogue of All Nations, World of Faith, Dunamis Church, Deeper Christian Life Ministry, Redeemed Christian Church of God na Life Gate Ministries.

Makanisa haya, na vituo vingine vya kuabudu, vinadai kutibu maradhi sugu kama vile kisukari, mikimbio ya damu, kiharusi, magonjwa ya moyo, kansa, Ukimwi miongoni mwa magonjwa mengine.