Kimataifa

Marais wa EU waapa kuganda na Ukraine kukiwa na hofu ya Trump kupumbazwa na Putin

Na REUTERS August 12th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

BRUSSELS, UBELGIJI

VIONGOZI 26 wa Umoja wa Bara Ulaya (EU) wamesema kuwa Ukraine lazima iwe huru kuamua mustakabali wake huku Rais wa Amerika Donald Trump na mwenzake wa Urusi Vladimir Putin wakitarajiwa kuandaa mazungumzo mnamo Ijumaa.

Rais Volodymyr Zelenskiy na viongozi wa EU watakuwa wakizungumza na Trump Jumatano kabla ya kuandaa kongamano lao jijini Alaska.

Kuna hofu kuwa Trump ambaye amekuwa akihakikisha Amerika inaipa Ukraine silaha, anaweza kulegeza kamba na kuridhia matakwa mengi ya Urusi katika mkutano wa Ijumaa.

“Mazungumzo ya maana yanaweza kuendelea tu wakati ambapo mapigano yamesitishwa ili kupunguza uhasama,” ikasema taarifa ya viongozi wa EU bila Hungary pekee.

“Tunaunga maafikiano ambayo yatahakikisha kuwa maslahi na haki za Ukraine zinalindwa pamoja na usalama wake,” ikaongeza taarifa hiyo.

Ukraine na EU zina hofu kuwa Trump ambaye analenga sana amani, huenda akalalia Ukraine na kutunuku juhudi za Urusi za miaka 11 za kutaka sehemu ya ardhi ya Ukraine.

“Sote tunataka Ukraine imara ambayo inaweza kujilinda na kujiendeleza,” ikasema taarifa hiyo huku EU ikisisitiza ipo tayari kufanya lolote kuhakikisha uhuru na ardhi ya Ukraine haivurugwi.

Hata hivyo, Waziri Mkuu wa Hungary Viktor Orban mwandani wa Putin alipinga taarifa ya wenzake wa EU.

“Inasikitisha kuwa EU ilitelekezwa na kile ambacho ni kibaya zaidi ni iwapo tutaanza kuyatoa maagizo tukiwa pembeni,” akasema Orban kupitia mtandao wake wa X.

“Kile ambacho viongozi wa EU wanaweza kufanya ni kuanzisha kongamano la EU-Urusi kama tu linalokuja la Amerika-Urusi,” akaongeza.

Trump amekuwa akijisawiri kama anayelemea Urusi huku akikubali kuipa Ukraine silaha zaidi na kutishia kuwekea Urusi vikwazo vya kiuchumi pamoja na mataifa yanayonunua mafuta yake.

Hofu ni kuwa kongamano la Amerika-Urusi litakuwa likifanyika Amerika na Trump anaweza kuweka maslahi ya Amerika mbele kuliko yale ya Ukraine.

Trump amekuwa akisema kuwa mkataba wa amani utahusisha Urusi na Ukraine kila upande kuachiliwa na kubadilisha baadhi ya sehemu za mpaka wao.

Hata hivyo, EU imekuwa ikisisitiza kuwa maeneo yote yanayozozoniwa ni ya Ukraine na hawaelewi jinsi ambavyo yataendea Urusi.

Urusi mnamo Jumatatu ilisema kuwa ilitwaa vijiji viwili mashariki mwa eneo la Summy, kupitia mapambano ya jeshi.

Kamanda wa Jeshi la Ukraine Oleksandr Syrskyi alikiri kuwa majeshi yao yanalemewa lakini akasema wanapambana kukabiliana na adui.

Urusi ilivamia Ukraine mnamo Februari 2022 lakini imekuwa ikiendesha vita vikali Summy baada ya Putin kutoa amri kuwe na mpaka ambao haukanyagwi na vikosi vya nchi yake pamoja na Ukraine.