Mazishi ya ‘kimasikini’ ya Buhari yashangaza wanamitandao wa Kenya
ALIYEKUWA Rais wa Nigeria, Muhammad Buhari alizikwa nyumbani kwake kaskazini mwa jimbo la Katsina, huku baadhi ya wakazi wakipanda mitini kufuatilia hafla ya kumwaga kiongozi huyo.
Buhari, aliyekufa mnamo Jumapili akiwa na umri wa miaka 82, alizikwa katika mazishi ya kikawaida mno, jambo lililofanya baadhi ya wazungumzaji mitandaoni kubaki na mshangao.
Hakuwekwa kwenye sanduku, na kaburi lake lilikuwa la udongo, kinyume na kawaida ya wanavyozikwa viongozi mashuhuri ambao huwekwa kwenye majeneza ya bei ghali pamoja na makaburi kujengwa kwa simiti.

Buhari alikuwa akipokea matibabu katika hospitali moja jijini London, Uingereza kabla ya kuaga dunia.
Aliwahi kukaa hospitalini Uingereza kwa zaidi ya siku 100 akiugua alipokuwa rais.
Kiongozi huyo, aliyeongoza Nigeria kati ya 2015 na 2023, ni mmoja wa marais wawili wa zamani wa kijeshi walirejea mamlakani kwa uchaguzi wa kidemokrasia.
Katika mji wake wa nyumbani wa Daura, wafuasi waliimba wakimtaja kama “Sai Baba” (Baba Wetu) huku wakijaribu kutazama jeneza lake likiteremshwa kaburini.
Rais Bola Tinubu aliwaongoza maafisa wa serikali kulipokea jeneza lenye mwili wa Buhari katika uwanja wa ndege wa Katsina. Pia walikuwepo wanaume na wanawake waliovalia mavazi ya Kiislamu.
Mizinga 21 ililipuliwa kwa heshima ya mwendazake katika uwanja huo wa ndege kabla ya mwili kusafirishwa kwa barabara hadi mji wa Daura.