Mbunge mmoja TZ naye kapendekeza hatua kali dhidi ya Wakenya
Na CHARLES WASONGA
MBUNGE mmoja wa Tanzania ametisha kuwachapa na kuwafurusha Wakenya wanaoishi nchini humo kufuatia tisho lililotolewa na Mbunge wa Starehe Charles Njagua dhidi ya Raia wa nchini hiyo.
Kwenye video iliwekwa katika mtandao wa Twitter, mbunge huyo aliyejawa na hamaki aliwahimiza wenzake wasiogope kushughulikia matamshi ya Bw Njagua, ya kuwavamia na kuwarufusha wageni wanaoendesha biashara nchini Kenya.
Mbunge huyo, ambaye jina lake halikutambuliwa mara moja, alikuwa akiongea katika kikao cha bunge la taifa la nchi hiyo ambapo matamshi ya Bw Njagua yalijadiliwa kwa kina.
“Kuna mbunge mmoja aliyetoa vitisho hivyo, ilhali tunatumia muda wote kumjadili. Mbunge mmoja wetu anaweza kutoa mwelekeo kuhusu suala hili na nitamuunga mkono,” akasema.
Hata hivyo, alitoa pendekezo kuhusu namna suala hilo linapaswa kushughulikiwa. Na akasema hivi:”Mheshimiwa spika, tusiharibu muda wetu kujadili jambo hili. Mimi mwenyewe nitaamrisha ya kwamba, tuwapige Wakenya wote ambao wanafanya kazi huku Tanzania kisha tuwarudishe kule kwao Kenya. Tusijadili jambo hili zaidi; huu ni woga!”
Hisia mseto
Kauli hii iliibua hisia mseto miongoni mwa wabunge huku wengine wakiishabikia kwa makofi lakini wengine wakiipinga hatua kama hiyo.
“Mheshimwa mbunge, tafadhali keti, tumesiki fikra zako,” Spika Job Ndugai akamwambia mbunge huyo aliyeonekana mwenye hamaki.
Mnamo Jumatatu Bw Njagua, maarufu kama Jaguar, alitisha kuwatumia vijana kuwakamata wageni wote wanaoendesha biashara Nairobi, kuwachapa, kisha kuwasindikiza hadi uwanja wa ndege ili warejee makwao.
Jumatano, mbunge huyo wa Starehe alikamatwa nje ya majengo ya bunge na kupelekwa katika kituo cha polisi cha Nairobi kuhojiwa kuhusu matamshi yake ya uchochezi dhidi ya wageni.