• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 10:50 AM
Mfalme ashangaza kumuoa mlinzi na kumfanya malkia

Mfalme ashangaza kumuoa mlinzi na kumfanya malkia

MASHIRIKA Na PETER MBURU

MFALME wa Thailand amemuoa naibu msimamizi wa masuala ya usalama wake na kumpa jina malkia, ujumbe kutoka kasri lake umesema.

Tangazo hilo limekuja kabla ya sherehe za kumvisha taji mfalme huyo kuanza Jumamosi, siku ambayo kiti chake kilitawazwa.

Mfalme Maha Vajiralongkorn mwenye umri wa miaka 66 alichukua wadhifa wa ufalme huo, kikatiba, baada ya babake kufariki mnamo 2016.

Ameoa na kutaliki mara tatu mbeleni na ana watoto saba.

Ujumbe kutoka kasri lake ulisema mfalme Vajiralongkorn “ameamua kumpandisha mamlaka Jenerali Suthida Vajiralongkorn Na Ayudhya, mlinzi wake, kuwa Malkia Suthida, na kuwa atakuwa na jina hilo la kifalme, sawa na hadhi ya familia hiyo ya kifalme.”

Suthida amekuwa na uhusiano wa muda mrefu na Mfalme Vajiralongkorn, wakionekana mbele ya umma kwa miaka mingi, japo uhusiano baina yao haujawahi kutambuliwa kwa njia rasmi.

Kanda za kuwaonyesha wakifunga ndoa zilichezwa na runinga moja Jumatano jioni, zikionyesha watu wa familia ya mfalme huyo na washauri wake wakihudhuria.

Mfalme huyo alionekana akimmiminia maji matakatifu Malkia Suthida kichwani, kisha wakatia sahihi cheti cha kufunga ndoa.

Vajiralongkorn alimteua Suthida Tidjai kuwa naibu msimamizi wa walinzi wake mnamo 2014, baada ya kuwa mhudumu wa ndege. Desemba 2016, alimpandisha madaraka kuwa jenerali katika jeshi.

Mfalme aliyetangulia, babake, alitawala kwa miaka 70, akiweka rekodi kama mfalme aliyetawala kwa miaka mingi zaidi duniani, hadi alipokufa 2016.

  • Tags

You can share this post!

Aua mtoto kwa kupoteza Sh135

Ndani miaka 4 kwa kumkata sikio aliyesalimia mkewe

adminleo