Mfalme awataka raia wasichinje kondoo Eid-al-Adha
RABAT, MOROCCO
MFALME Mohamed VI wa Morocco jana aliwataka raia wa taifa hilo wajizuie kuwachinja kondoo wakati wa sikukuu ya kuchinja maarufu kama Idd-ul-Adha mwaka huu.
Kauli ya Mfalme Mohamed VI inatokana na ukame mkali ambao upo Morocco na umesababisha idadi ya mifugo nchini humo ipungue. Idd-ul-Adha ni kati ya sikukuu mbili muhimu kwenye dini ya Kiislamu kando na ile Idd-ul-Fitr.
Idd-ul-Adha mwaka huu itakuwa Juni 6-Juni 7 na huku mfungo wa Idd-ul-Fitr ukianza Jumamosi hii na kukamilika Aprili 1.
Sikukuu ya kuchinja huwa ni ya kukumbuka na kuenzi jinsi Ibrahimu alivyokuwa tayari kumtoa mwanawe Isaka kafara. Hata hivyo, kutokana na imani yake dhabiti iliyokuwa ikipimwa, mwenyezi alimshukishia kondoo na akamwaachilia Isaka akamchinja mnyama huyo.
Waislamu huadhimisha siku hiyo kwa kuwachinja kondoo au mbuzi kisha nyama hiyo hugawanywa miongoni mwa familia na pia maskini hunufaikia ukarimu huo.
Idadi ya ng’ombe na kondoo imepungua kwa asilimia 38 mnamo 2025 Morocco tangu hesabu ya mwisho miaka tisa iliyopita.
“Tunamakinikia kuhakikisha tunatimiza hitaji hili muhimu la kidini ila pia tuangalie uchumi wa nchi yetu na mabadiliko ya tabianchi. Idadi ya mifugo yetu imepungua sana,” akasema Mfalme kwenye barua iliyosomwa kwa niaba yake na Waziri wa Masuala ya Nje Ahmed Taoufiq kwenye runinga ya serikali.
“Kuchinja wakati wa Idd-ul-Adha kutakuwa na athari kubwa kwa watu wetu ambao uwezo wao wa kiuchumi umeshuka,” ikaongeza taarifa ya Mfalme.
Kwa kipindi cha miaka 30, mvua imepungua sana mwaka huu Morocco tena kwa asilimia 53 na kusababisha ukosefu wa nyasi kwa mifugo. Kiwango cha nyama pia kimepungua na kupandisha bei kwenye masoko ya Morocco, taifa hilo likilazimika kuagiza kutoka nchi nyingine.
Hivi majuzi, Morocco ilitia saini mkataba wa kuagiza kondoo 100,000 kutoka Australia.
Katika bajeti ya 2025, Morocco iliondoa ushuru kwenye nyama ya ngómbe, kondoo na ngamia ili kudhibiti bei kwenye masoko yake.