Kimataifa

Mgombea urais wa Zanzibar atiwa mbaroni, Lissu apinga matokeo

October 29th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na WAANDISHI WETU

MGOMBEAJI urais kisiwani Zanzibar kwa tiketi ya chama cha upinzani cha ACT Wazalendo, Maalim Seif Sharif Hamad, alikamatwa na polisi Alhamisi punde baada ya kuhutubia kikao cha wanahabari.

Katika uchaguzi wa Tanzania bara, mgombeaji wa urais kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu alitangaza kuwa hatatambua matokeo ya Uchaguzi Mkuu uliofanyika Jumatano akidai ulikumbwa na dosari nyingi.

Jana ilikuwa ni mara ya pili kwa Maalim Seif kukamatwa na polisi wiki hii. Alikamatwa mara ya kwanza Jumanne asubuhi alipokuwa ametembelea kituo cha upigaji kura cha Garagara kilicho Unguja wakati maafasa wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar walipokuwa wakipiga kura.

Katika mahojiano kwa njia ya simu, Kamishna wa Polisi Zanzibar, Mohamed Haji Hassan alisema ilikuwa mapema kuchapisha habari hizo kwani walikuwa bado wanafanya uchunguzi kuhusu suala hilo.

“Polisi wamekamata viongozi wote wa ACT Zanzibar na mmoja wa viongozi alipigwa hadi karibu kufariki. Hatuna uhakika kama bado yuko hai kwa vile alitiwa mbaroni,” Kiongozi wa ACT, Zitto Kabwe akasema kupitia mtandao wa Twitter.

Awali, Bw Zitto alituma ujumbe kuhusu kukamatwa kwa Nassor Mazrui, ambaye ndiye Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho na pia msimamizi wa kampeni zake Zanzibar katika uchaguzi wa mwaka huu.

Kwa mujibu wa katibu wa uhusiano wa umma katika chama hicho, Salum Bimani, kuna maafisa wengine saba wa chama ambao walikamatwa akiwemo Issa Kheri Hussein, ambaye ni katibu wa kibinafsi wa Maalim Seif.

Mgombea urais wa Zanzibar kwa tiketi ya ACT- Wazalendo, Maalim Seif Sharif Hamad akipiga kura katika kituo cha Garagara jimbo la Mwera mkoa wa Mjini Magharibi Unguja. Picha na Bakari Kiango|Mwananchi, Tanzania

Hayo yalitokea wakati ambapo mgombeaji urais kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Dkt Hussein Mwinyi alikuwa akiongoza katika matokeo ya kura ya mapema, akifuatwa na Maalim Seif, kwa mujibu wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC).

Kwenye video iliyosambazwa katika mitandao ya kijamii, Maalim Seif alionekana akitoa wito kwa Wazanzibari kukutana katika barabara ya Michenzani iliyo katika kisiwa cha Unguja ili wapinge kile walichokitaja kuwa uvurugaji wa mfumo wa uchaguzi.

“Iwe kama viongozi watakufa au kukamatwa, tuko tayari kwa lolote lile,” alisema Maalim Seif katika video hiyo.