Kimataifa

Mhadhiri taabani kwa kumtusi Museveni

November 7th, 2018 Kusoma ni dakika: 1

MASHIRIKA NA PETER MBURU

POLISI nchini Uganda bado wanawazia kumshtaki mwanaharakati na msomi ambaye ana umaarufu mkubwa mitandaoni, kwa kumtusi Rais Yoweri Museveni.

Msemaji wa polisi Vincent Ssekatte alisema kuwa Bi Stella Nyanzi anakabiliwa na hatia ya kutumia “chapisho la matusi” katika akaunti yake ya Facebook na kumuita rais Museveni  ‘makalio’.

Polisi wanasema kuwa Bi Nyanzi alitumia matamshi ya matusi kwa Rais Museveni na mamake.

Hata hivyo, mawakili wa mwanaharakati huyo wamesema kuwa bado hawajafahamishwa kuhusu mashtaka ambayo anakumbana nayo.

Bi Nyanzi ambaye alikuwa mtafiti katika chuo kikuu cha Makerere hadi Machi 2017 na ambaye amekuwa akitetea maslahi ya wanyonge na wanawake alitumia picha za grafiki na maneno yaliyomrejelea Rais Museveni kama “matako”.

Mwanamke huyo aidha amewahi kufanya maandamano yake peke yake akiwa uchi nje ya ofisi yake, wakati alipotumwa katika likizo ya lazima na chuo kikuu cha Makerere.

Hiyo ilikuwa baada ya kumtusi mkewe Rais Museveni, ambaye pia ni waziri wa elimu, na kumlaumu kuwa hakuwa akifanya kazi yake ipasavyo.

Lakini mwezi uliopita, jopokazi iliyoundwa kumchunguza ilipendekeza arudishwe kazini mara moja na alipwe mshahara wote wa tangu aliposimamishwa, japo hilo halijatendeka.