Mimi si Mnigeria, mwanasiasa wa Uingereza akana asili yake
KIONGOZI wa chama chenye itikadi kali, Kemi Badenoch, amesema hajitambulishi tena kama raia wa Nigeria na kwamba hata hana pasipoti ya nchi hiyo.
Badenoch alizaliwa Uingereza na kulelewa Nigeria na Uingereza kabla ya kurejea nchini humo akiwa na umri wa miaka 16 kwa sababu ya hali mbaya kisiasa na kiuchumi Nigeria pamoja na kujiendeleza kielimu.
Akizungumza katika kituo cha mbunge wa zamani na mtangazaji wa televisheni, Gyles Brandreth, Rosebud Podcast, alisema yeye ni “Mnigeria kupitia asili. Lakini kwa “kitambulisho, mimi si Mnigeria kwa hakika”.
Badenoch, aliyeishi mbeleni jijini Lagos, alizungumza kwa kina kuhusu malezi yake.
“Ninajua taifa hilo vyema, nina jamaa wengi wa familia humo, na ninavutiwa zaidi na kinachoendelea huko,” alisema.
“Lakini nyumbani ni mahali familia yangu ya sasa imo.”
Kuhusu kukosa kuchukua pasipoti mpya, alisema: “Sijitambulishi nayo tena. Sehemu kubwa ya maisha yangu imekuwa Uingereza na sijawahi tu kuhisi haja ya kufanya hivyo kamwe.”
“Mimi ni Mnigeria kupitia asili, kuzaliwa, licha ya kutozaliwa humo kwa sababu ya wazazi wangu… kwa utambulisho, kwa hakika mimi si Mnigeria.”
Badenoch alisema alipozuru nchi hiyo baba yake alipokufa, alilazimika kupata hati ya kusafiri, mchakato uliokuwa “kitendawili kigumu.”
Alisema tajriba yake ya mapema Nigeria iliunda mtazamo wake kisiasa ikiwemo “sababu inayofanya nisipende ujamaa.”
Kama mtoto,”Nakumbuka sikuwahi kamwe kuhisi nafaa kuwepo huko,” alisema,” akielezea kukumbuka “aliporejea Uingereza 1996 na kuwaza: hapa ni nyumbani.”
Kiongozi huyo wa Tory alisema sababu iliyomfanya kurejea Uingereza “ni ya kuhuzunisha mno.”
“Ni kwa kuwa wazazi wangu waliwaza: ‘Hakuna mustakabali kwako taifa hili.’”
Alisema hajapitia ubaguzi wa rangi Uingereza “katika namna yoyote yenye maana,” alisema “nilijua naenda mahali nitakapoonekana tofauti na kila mtu, na sikufikiri hilo ni jambo lisilo la kawaida.
Mwishoni mwa 2024, Badenoch alikashifiwa kwa kusema alikua kwa hofu na ukosefu wa usalama Nigeria ilipokuwa imekolea ufisadi.
Naibu rais Nigeria Kashim Shettima alijibu kwamba serikali yake “inajivunia” Badenoch “licha ya juhudi zake za kudhalilisha taifa la asili yake.”
Alimkashifu Badenoch akisema “amedunisha” taifa hilo la Afrika Magharibi.