Mjisajili ili muokolewe, serikali yaambia Wakenya wanaotoroka vita Lebanon
HUKU hali ya usalama ikiendelea kudorora zaidi nchini Lebanon, Serikali ya Kenya imewataka Wakenya nchini humo kujisajili waokolewe.
Kwenye taarifa, Wizara ya Masuala ya Kigeni na Masilahi ya wanaoishi ughaibuni inasema idadi kubwa ya Wakenya hawajajisajili huku hali ikiendelea kuwa mbaya Israel ikizidisha mashambulio katika ngome za Hezbollah.
“Ili kuhakikisha usalama na kuondolewa kwa raia wetu, tunawahimiza Wakenya walioko Lebanon kujisajili nasi. Ni wale waliojisajili nasi pekee watakombolewa,” ikasema taarifa hiyo iliyotolewa Jumatano, Oktoba 2, 2024.
Wizara hiyo imewataka Wakenya hao kuwa wamejisajili kabla ya Oktoba 12, 2024.
“Kufuatia kudorora kwa usalama Lebanon, wizara hii inatoa hakikisho kuwa imeupa kipaumbele usalama wa Wakenya kwa kuhakikisha kuwa wanarejeshwa nyumbani wakiwa salama,” taarifa hiyo ikaongeza.
Kando na hayo, serikali ya Kenya imeelezea kujitolea kwa kushirikiana na mashirika ya kimataifa na yale ya Lebanon kuhakikisha kuwa Wakenya wanasaidiwa kujisalimisha.
Kufikia sasa, Wizara ya Masuala ya Kigeni imeyakomboa makundi mawili ya Wakenya kutoka taifa hilo la Mashariki ya Kati.
Mnamo Agosti 6, 2024 Kenya ilianzisha mpango wa dharura wa kuwaondoa raia wake nchini Lebanon, kutokana taharuki iliyosababishwa na mapigano kati ya Israel na kundi la wapiganaji la Lebanon.
Hapo ndipo Wizara iliwashauri Wakenya kujisajili ili waokolewe au wahamie maeneo salama wakiweza kufanya hivyo.
Aidha, Wizara hiyo ilitoa nambari ya dharura isiyolipiwa ambayo Wakenya wenye jamaa zao Lebanon wanaweza kutumia kusaka usaidizi. Nambari hiyo ya simu ni: 254114757002.
Wiki moja iliyopita, Wakenya wengi walioko Lebanon walilalamika kutelekezwa na serikali huku maisha yao yakiwa hatarini.
Waliomba warejeshwe nyumbani wakihofia kuuawa katika vita vilivyochacha kati ya Israel na kundi la Hezbollah.
Inakadiriwa kuwa jumla ya Wakenya 26, 599 wanaishi Lebanon.
Balozi wa Kenya nchini Lebanon Halima Mohamud, anayehudumu kutoka Kuwait alinukuliwa akisema afisi yake huwasiliana na Wakenya walioko Lebanon na imewapa nambari ya simu wanayoweza kutumia kumfikia endapo watakumbwa na hatari.
“Hakuna Mkenya aliyekufa wala kujeruhiwa. Tunawasiliana nao kila mara kujua hali yao,” akaeleza.