Kimataifa

Mkataba ni karatasi tu? Waasi wa M23 wazidi nguvu jeshi la DRC na kuteka mji muhimu

Na WINNIE ONYANDO, MASHIRIKA December 11th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

KINSHASA, DR CONGO

KUNDI la waasi wa AFC/M23 wanaoungwa mkono na Rwanda wamechukua udhibiti wa mji wa kimkakati wa Uvira unaopakana na Burundi baada ya mapigano makali kuzuka kati yake na Jeshi la Congo la FARDC.

Kumeripotiwa mapigano makali na milipuko ya mabomu Jumanne usiku kabla ya waasi wa M23 kufanikiwa kuingia na kuchukua udhibiti wa mji wa kimkakati wa mashariki mwa DRC wa Uvira, jambo lililowafanya maelfu ya raia wa Congo kukimbilia katika nchi jirani ya Burundi.

Hata hivyo, baadhi ya walioshuhudia tukio hilo walisema kuwa mapigano yalikuwa yakiendelea katika baadhi ya maeneo ya mji huo.

Kulingana na vyanzo mbalimbali vya kiusalama na kijeshi, wanamgambo hao waliingia Uvira wakitokea eneo la kaskazini, huku Amerika na mataifa kadhaa ya Ulaya yakiwahimiza waasi wa M23 kusimamisha mara moja mashambulio yao na kuitaka Rwanda kuwaondoa wanajeshi wake kutoka eneo hilo la mashariki mwa DRC lenye utajiri mkubwa wa madini.

Wakati M23 ikichukua udhibiti wa ngome kubwa ya mwisho katika jimbo la Kivu Kusini, wanajeshi wengi wa Congo walijichanganya na raia waliokimbilia Burundi, nchi iliyokuwa imewatuma wanajeshi wake kusaidia DRC kupambana na Rwanda.

Chanzo kimoja kutoka serikali ya Burundi kilisema kwamba katika kipindi cha siku mbili zilizopita, zaidi ya watu 8,000 wamewasili nchini humo kutoka Congo na kwamba serikali haina uwezo wa kuwahudumia iwe kwa chakula au huduma za matibabu.

Shirika la Kimataifa la Kuwahudumia Wakimbizi (UNHCR) limesema kuwa katika kipindi cha wiki moja pekee takriban watu 30,000 wameingia nchini Burundi huku Umoja wa Mataifa (UN) ukisema mapema wiki hii kuwa watu 200,000 wameyakimbia makazi yao mashariki mwa Congo katika siku za hivi karibuni.

Shambulio la hivi punde la M23 linajiri takriban mwaka mmoja tangu kundi hilo linaloungwa mkono na Rwanda kuchukua udhibiti wa miji muhimu ya Goma na Bukavu, katika eneo ambalo limekumbwa na machafuko kwa zaidi ya miongo mitatu.

Katika taarifa iliyotolewa Jumatatu jioni, Umoja wa Mataifa ulisema takriban watu 74 wameuawa, wengi wao wakiwa raia, na 83 wamelazwa hospitalini wakiwa na majeraha kutokana na kuongezeka kwa mapigano katika eneo hilo katika siku za hivi karibuni.

Mjini Washington, Amerika na wanachama wengine tisa wa Kundi la Kimataifa la Mawasiliano (ICG) walionyesha “wasiwasi mkubwa” kuhusu ghasia zilizozuka upya.

Ilisema mashambulio mapya ya waasi wa M23 “yana uwezo wa kuyumbisha uthabiti wa eneo zima” na kuongeza kuwa kuongezeka kwa matumizi ya ndege zisizo na rubani na za mabomu ya kujitoa mhanga yanaashiria ongezeko kubwa la mapigano na kuwa tishio kubwa kwa raia.

Serikali ya Rwanda hata hivyo imekuwa ikipinga madai kuwa inaunga mkono waasi wa M23.